2014-06-02 08:48:35

Yesu yupo pamoja nanyi!


Mama Kanisa anaadhimisha Siku kuu ya Kupaa Bwana Mbinguni, siku arobaini baada ya ufufuko wake na hapo wafuasi wa Kristo wanatumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Yesu anakwenda kwa Baba yake wa mbinguni na mitume wanatumwa kwenda ulimwenguni kote kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo kwa kutambua kwamba, Yesu mwenyewe amewaahidia wafuasi wake kwamba, ataendelea kuwa pamoja nao hadi ukamilifu wa dahali!

Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari Siku kuu ya Kupaa Bwana mbinguni, tarehe 1 Juni 2014 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican anasema kwamba, Yesu amepaa kwenda kwa Baba yake wa mbinguni ili kuwaandaliwa mitume wake nafasi, lakini pia anaendelea kuonesha uwepo wake katika matukio mbali mbali ya maisha ya mwanadamu kwa njia ya nguvu ya Roho Mtakatifu na kuwanyanyua pale wanapoteleza na kuanguka; wanaponyanyaswa na kudhulumiwa.

Baba Mtakatifu anasema, zawadi kubwa ambayo Yesu amempelekea Baba yake wa mbinguni ni madonda yake matakatifu, alama ya upendo na huruma ya Mungu kwa binadamu, changamoto na mwaliko kwa waamini kukimbilia huruma ya Mungu isiyokuwa na kifani katika maisha yao, kwani Mwenyezi Mungu yuko tayari kuwapokea na kuwasamehe dhambi zao.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, Yesu yuko pamoja na Kanisa lake, ili kuendeleza utume wake kwa kuwafundisha na kuwabatiza watu katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kanisa limezaliwa na linatumwa kwenda kuwatangazia watu Habari Njema ya Wokovu, kila mtu anapaswa kutekeleza dhamana hii kadiri ya nafasi na uwezo wake.

Kwa mitume wake ambao wanatekeleza dhamana yao kama Wamissionari sehemu mbali mbali za dunia, Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha kwamba, Yesu yuko pamoja nao ili kuwatia shime katika kazi zao kwani rasilimali watu, nguvu, miundo mbinu ni muhimu lakini bila uwepo wa Roho Mtakatifu, mambo yote haya hayafui dafu! Wakristo wawe na ujasiri wa kumtangaza Kristo kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao na kwamba, Bikira Maria anaendelea kufanya hija na Wafuasi wa Kristo, kwani ni Mama wa matumaini!







All the contents on this site are copyrighted ©.