2014-06-02 10:39:48

Washeni moto wa Injili kwa utakatifu wa maisha!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili jioni tarehe 1 Juni 2014 ameshiriki katika kongamano la Chama cha Kitume cha Uamsho wa Kikatoliki kwa kuwakumbusha kwamba, wamebahatika kupata zawadi kubwa kutoka kwa Kristo na mafuriko ya neema yanayowawezesha kuwa watu wapya katika Kristo kwa njia ya Roho Mtakatifu anayewakirimia karama na mapaji mbali mbali kwa ajili ya huduma kwa Kanisa katika hali ya amani na utulivu!

Amewataka wanachama wote kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa kidugu kwa kutambua kwamba, Yesu Kristo ndiye kiongozi mkuu na wengine wote wanatumwa kuhudumia kwa unyenyekevu. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, mwanzoni hakuwapenda wanachama wa Chama cha Uamsho kwani kutokana na mtindo wao wa sala na ibada walionekana kana kwamba, ni shule ya samba. Lakini baadaye amewaelewa na kuwasaidia kukua na kukomaa katika maisha yao ya kiroho tangu akiwa nchini Argentina.

Baba Mtakatifu anasema, Chama hiki ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa hususan katika kuwatangazia watu Injili ya Furaha na kuwashirikisha wengine upendo wa Mungu usiokuwa na kifani unaojifunua kwa njia ya Maandiko Matakatifu, changamoto ya kupenda kusoma, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha! Anawataka wanachama hawa kumwachia Mungu nafasi katika maisha yao na kamwe wasiwe ni kikwazo cha neema ya Mungu kwa watu wake.

Baba Mtakatifu anawakumbusha kwamba, Kanisa limewapatia nyaraka muhimu ambazo zinaweza kuwasaidia katika hija ya maisha yao ya kiroho kwa kuwa na mwelekeo sahihi wa kitaalimungu na katika shughuli za kichungaji; Karama za Roho Mtakatifu mintarafu majadiliano ya kiekumene na Chama cha Uamsho wa Roho Mtakatifu katika huduma kwa binadamu. Kwa ufupi Baba Mtakatifu anasema, Chama hiki cha kitume kinatumwa kuinjilisha, kujadiliana na kuhudumia hasa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baba Mtakatifu anategemea kuwaona wanachama wanaotolea ushuhuda wa upendo kwa Mungu kwa kuishi kadiri ya Kweli za Kiinjili pamoja na kujikita katika utakatifu wa maisha. Anawaalika kushirikishana neema ya Ubatizo inayobubujika kutoka kwa Roho Mtakatifu na kwamba, anawategemea kuwa Wainjilishaji wakuu kwa kutumia Neno la Mungu, lakini kubwa zaidi kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao, wakiwa wameungana na kushikamana katika huduma kwa maskini.

Baba Mtakatifu anawataka wanachama hawa kuanza maandalizi ya mkutano wa kimataifa utakaofanyika mwezi Juni, 2015 kwa kuwashirikisha Mapadre kutoka katika Chama hiki cha Kitume na kwamba, anatarajia, Mungu akipenda, kuonana nao tena kunako Mwaka 2017 wakati wa kuadhimisha Jubilee ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa chama cha Uamsho wa Kikatoliki ndani ya Kanisa, matunda ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.