Upendo unajikita katika uaminifu, udumifu na kuzaa matunda!
Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu kwenye
Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Siku ya Jumatatu tarehe 2 Juni
2014 amesema kwamba, upendo unaorutubisha maisha ya Kanisa kutoka kwa Kristo mwenyewe
unajikita katika uaminifu, udumifu na unaozaa matunda!
katika Ibada hii kulikuwepo
na wanandoa waliokuwa wanaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 25, miaka 50 na miaka 60
tangu walipofunga Sakramenti ya Ndoa Kanisani na kwamba, walipenda kumshukuru Mungu
wakiwa wameungana na Baba Mtakatifu Francisko ambaye anaendelea kutoa kipaumbele cha
pekee katika maisha na utume wa Ndoa na familia. Baba Mtakatifu amewataka wanandoa
hawa kuendelea kuwa waaminifu, kwa kudumu katika Sakramenti ya Ndoa na kuendeleza
matunda ya Sakramenti hii ambayo ni watoto, zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Baba
Mtakatifu anasema, Yesu alionesha upendo wa dhati kwa Kanisa lake na kuutolea ushuhuda
makini. Uaminifu na upendo wa Kristo kwa Kanisa lake ni mwanga katika Sakramenti ya
Ndoa. Yesu kamwe hachoki kuonesha upendo kwa Kanisa lake hata katika nyakati za magumu
na majaribio ya maisha. Upendo kati ya wanandoa ujioneshe kwa namna ya pekee katika
kusaidiana na kutatua matatizo na changamoto katika umoja na mshikamano, ili kuendelea
kuenzi tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.
Upendo wa Kristo unaliwezesha
Kanisa kupata watoto wapya wanaozaliwa kwa maji na Roho Mtakatifu. Hata katika maisha
ya ndoa na familia watu wanaweza kukirimia watoto wenye afya nzuri au hata wakati
mwingine watoto ambao afya zao si nzuri sana, lakini wote hawa ni zawadi kutoka kwa
Mwenyezi Mungu. Inasikitisha kuona kwamba, kuna watu katika maisha ya ndoa na familia
hawapendi kupata watoto, wanaridhika kukaa katika upweke na kubembeleza paka au mbwa.
Fainali za ndoa kama hizi anasema Baba Mtakatifu ni uzee usiokuwa na matumaini, uzee
unaoelemewa na upweke na mawazo mabaya!