2014-06-02 08:46:43

Papa asikitishwa na vita inayoendelea huko Ukraine na Afrika ya Kati!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya tafakari na sala ya Malkia wa Mbingu katika maadhimisho ya Siku kuu ya Kupaa Bwana mbinguni, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, tarehe 1 Juni 2014 ameonesha masikitiko yake makubwa kutokana na maafa yanayoendelea kujitokeza huko nchini Ukraine na katika Jamhuri ya Afrika ya kati.

Baba Mtakatifu anawaalika wote wanaohusika kuvuka vikwazo vinavyopelekea wao kutoelewana na kuanza kujikita katika mchakato wa majadiliano ili kupata amani ya kudumu. Baba Mtakatifu ameungana na waamini pamoja na mahujaji waliokuwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kumwomba Bikira Maria Malkia wa amani ili aweze kusaidia mchakato wa amani katika mataifa haya ambayo yanaendelea kukabiliana na hali ngumu ya maisha!

Baba Mtakatifu Francisko amewakumbusha waamini na mahujaji kwamba, Jumamosi, iliyopita, Jimboni Collevalenza Kanisa limemtangaza Mtumishi wa Mungu Maria Josefa Alhama Valera, Mwanzilishi wa Shirika la Watawa watumishi wa Upendo wenye Huruma kuwa Mwenyeheri. Ushuhuda wa maisha yake, ulisaidie Kanisa kuendelea kutangaza huruma ya Mungu isiyokuwa na kifani kwa waja wake.

Katika maadhimisho ya Siku ya 48 Upashanaji Habari Ulimwenguni, iliyokuwa inaongozwa na kauli mbiu "Mawasiliano katika huduma ya kweli ya utamaduni wa kukutana", amekazia kwa mara nyingine tena umuhimu wa vyombo vya habari kusaidia mchakato wa ujenzi wa umoja katika familia ya binadamu, mshikamano pamoja na kutafuta maisha bora kwa wote. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kusali ili kwamba, mawasiliano yawe kweli ni kwa ajili ya huduma inayojenga na kuimarisha utamaduni wa watu, jamii na mataifa kukutana kwa kuzingatia heshima na utamaduni wa kusikilizana!







All the contents on this site are copyrighted ©.