2014-06-02 07:49:17

Moto wa Injili!


Chama cha Kitume cha Uamsho wa Kikatoliki, Jumapili tarehe 1 Juni 2014 kimewasha moto wa Injili mjini Roma kuwashirikisha maelfu ya waamini kutoka ndani na nje ya Italia. Limekuwa ni tukio la sala, tafakari na ushuhuda wa neema na baraka za Mungu kati ya watu wake. Waamini wametumia nafasi hii pia kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho.

Kardinali Angelo Comastri amezungumzia kuhusu umuhimu wa kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu kama kielelezo cha ushuhuda wa imani tendaji wakati huu Mama Kanisa anapojikita katika Uinjilishaji Mpya unaopaswa kujielekeza zaidi katika maisha adili na manyofu. Padre Raniero Cantalamessa ametafakari kuhusu umuhimu wa kumwamini Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu, chemchemi na kiini cha imani ya Kanisa.

Wanachama wa Chama cha kitume cha Uamsho wa Kikatoliki wamekumbushwa kwamba, wamempokea Roho Mtakatifu, ili awasaidie kuwa kweli ni mashahidi waKristo hadi miisho ya dunia. Kumbe, changamoto ni kuendeleza ujenzi wa ufalme wa Mungu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Roho Mtakatifu nikielelezo makini cha umoja na mshikamano wa dhati ndani ya Kanisa, kila mwamini akijitahidi kutumia vyema karama na mapaji aliyokirimiwa na Roho Mtakatifu kwa ajili ya sita na utukufu wa Mungu.








All the contents on this site are copyrighted ©.