2014-05-31 09:46:34

MSIBA!


Kulikoni kusherekea msiba! Endapo unashindwa kuelewa na unashangaa juu ya sikukuu ya kifo kadhalika ni vigumu sana kumfanyia sherehe mtu anayesafiri kwenda mbali mahali atakakokaa kwa muda mrefu. Tunapoagana na wapendwa ndugu zetu tunasikitika na tunatulizana kwa maneno kama haya: Kwa heri, Safari njema, Inshallah, Bye!


Somo la leo ni aya za sura ya mwisho kabisa ya Injili ya Mateo. Sehemu hii yaweza kuwa ni ufupisho wa historia ya maisha yote ya Yesu ambaye kwa muda mrefu aliishi Nazareti, baadaye akafanya makazi huko Kafarnaumu pwani ya ziwa la Galilea, kisha alienda Yerusalemu yalikomfika mauti na ndiyo ukawa mwisho wa habari. Tumekuja kutulizika pale Yesu alipofufuka. Leo lakini anatuaga anaondoka, nasi tunasherekea na kuita sikukuu ya kupaa. Kulikoni kumsherekea Yesu anayeondoka?


Sikukuu ya leo ambayo Yesu anaingia kwenye ulimwengu wa Mungu na makao ya Baba, siyo safari ya kumpa “kwa heri” au “kwa heri ya kuonana”. Safari hii ni ya “kuaga bila kuondoka.” Injili inaanza kwa kusema kwamba, mitume kumi na mmoja walikusanyika kwenye mlima ambao walielekezwa kwenda. Mlima huo ni ule wa heri nane. Hapa ndipo Yesu alipokutana mara ya kwanza na kikundi cha mitume. Mahali hapo ndipo alianzia kufanya kazi.


Yesu kama binadamu alikuwa na makazi yake Galilea na akitokea hapo aliweza kwenda sehemu mbalimbali kuhubiri. Pahala hapo basi ni pa kuanzia na pa kuishia safari. Ni mwisho wa uwanja na mwanzo wa uwanja mpya. Tungeweza pia kusema “Safari moja inaanzisha safari nyingine.” Kikundi kile cha mitume kumi na mmoja, kimeagizwa na Yesu kukutanika hapo.


Yuda anakosekana. Maelezo ya kukosekana Yuda aliyemsaliti Yesu yanaeleweka, lakini katika injili ya leo huyu Yuda anatoa fundisho mpya. Yuda anasimama kama ishara au alama ya mtu anayefanya mambo kinyume. Ni mtu asiyetaka kubadilika na anayeamua kufanya uchaguzi wake peke yake. Ni mtu anayetumia uhuru kama anavyotaka yeye.


Kumbe yule asiyepanda mlima ule wa Heri nane, hawezi kumwona Mfufuka, hawezi kupata mang’amuzi. Yuda ni mfano halisi wa mtu huyo aliyejitenga, anayeamua kubaki kushabikia ulimwengu wa kale, ulimwengu wa udanganyifu, ulimwengu wa biashara, ulimwengu wa kuuza na kununua, wa kujadiliana juu ya bei ya bidhaa mbalimbali, ulimwengu wa kupiga siasa za kidunia tu.


Hali halisi ya kikundi cha mitume kumi na mmoja ni tete, kimejaa mashaka, woga, na mitume wanajisikia kama jeshi lililopigwa vibaya sana na kujeruhiwa, limesambaratishwa na sasa linajaribu kujipanga upya. Kikundi hiki kinahitaji kutiwa nguvu ili kiweze kuanza upya. Sasa kimekusanyika hapa mlimani. Mwinjili Matayo anasema: “Nao walipomwona walimsujudia; lakini waliona shaka.” (28:17).


Neno hili “walipomwona”, halimaanishi kule kuona kwa macho ya kimwili, bali ni kule kufaulu kuona hatima ya yule aliyeweza kutoa maisha yake kwa ajili ya upendo. Kuona aina hiyo kunawezekana tu kwa wale waliokwea mlima ule wa heri. Kumbe yabidi kwanza kuupanda mlimani huo, halafu utaelewa kwamba hatima ya wale wanaopokea heri inayopendekezwa na mwalimu wao ndiyo hatima ya maisha kamili katika Mungu kama ilivyotokea kwa Yesu wa Nazareti.


Yesu anapowajia mitume: “Wanamsujudia”: Huko kusujudia maana yake kuelewa uwepo wa Mungu katika Yesu yaani kuionaa na kuipokea sura ya Mungu inayojionesha katika Yesu, Mungu anayejitoa mwenyewe katika Upendo ndani ya Yesu. Yasemwa pia kwamba mitume hawa “lakini waliona shaka.” Hapa unaona kwamba Kusujudia na Wasiwasi (woga) vinaenda sambamba katika wanafunzi hawa.


Woga na wasiwasi vinakwenda pamoja na imani. Huwezi kuepa wasiwasi. Hakutakuwa hata mara moja vithibiti vya imani, yaani katika upendo hakuna hoja na vithibiti vya kiakili. Hiyo ni hali halisi kabisa ya ubinadamu wetu. Ndiyo maana, Yesu hawagombezi na wala hajali tu, kwani anaona ni kitu cha kawaida kwa wanafunzi. Hatuwezi kuwa na hoja na vithibiti vya ufufuko wa Yesu, bali tunao uthibiti kutokana na mapendekezo aliyotuambia na kutufanyia Yesu mwenyewe kutokana na maisha yake.


Yesu angewagombeza sana endapo wanafunzi wangekuwa na uhakika kamili kabisa juu ya ufufuko, kwa sababu hatari kubwa ya kuwa na uhakika katika imani mapato yake ni kuwa na masimamo mkali katika dini, na kuwalazimisha wote kufuata itikadi za imani au dini yako.


Wanafunzi walikuwa na wasiwasi kutokana na mapendekezo ya Yesu mwenyewe aliyoyatoa kabla juu ya mlima uleule waliokusanyika. Wakizikumbuka zile heri nane wanaona zinakanganya na zinaletesha wasiwasi. Mathalani, juu ya kuwa maskini, juu ya kuonewa, juu ya kudhulumiwa. Mashaka yanakuja zaidi pale wanapojihoji na kujiuliza, “Hadi sasa tulikuwa tunamtegemea Yesu, kumbe sasa tumeishiana, hivi tumepoteza kila kitu. Mambo yote mazuri aliyofundisha yamekuwa ndoto za bure.” Yesu hatishiki, kwani anajua kwamba hawezi kuwa na hoja zinazoshikika mkononi kuhusu mapendekezo aliyotoa.


Mfuasi wa Kristu anaweza kuwa katika kundi la akina Yuda wasiotaka kubadili misimamo yao ya maisha na kumfuata Yesu. Lakini wale walio katika imani na wanaomwabudu Yesu, hawatakosa kuwa na mashaka kama mitume. Kwa maana hiyo, inabidi kila siku kuilisha imani yetu kwa Neno la Mungu. Tusipokuwa juu ya mlima wa heri na badala yake tukashuka huko chini tutakuwa katika hali halisi ya maisha ya ulimwengu, utaanza kuamini juu ya kile kinachooneka.


Yesu akawaambia: “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.” Katika vishawishi vyake kule jangwani shetani alimpendekezea Yesu kuupata ulimwengu wote akimsujua. Ukifuata mantiki yake angeweza kuuteka ulimwengu wote na kuutawala. Kumbe mamlaka hayo Yesu aliyakataa kwani yeye alikuwa na mamlaka ya “mbinguni na duniani”. Nayo siyo mamlaka ya kutawala, bali ni ya kutoa maisha na ya kuokoa.


Haya ndiyo mamlaka kwa ajili ya kuanza upya maisha. Hivi anawaagiza “Enendeni” yaani kuanza safari ya kutembea. Kwa hiyo, hatima ya injili ya Mateo ni mwanzo wa injili nyingine pamoja na Kristu mfufuka. Hatima ya maisha ya Yesu siyo mwisho bali ni mwanzo. Kazi iliyoko ni “kuwafanya mataifa yote kuwa wanafunzi.” Maana yake kuwafanya kuwa wasikilizaji, na wapokeao wa mapendekezo haya ya Heri.


Haitoshi hiyo nadharia ya kufundisha wanafunzi, bali “Mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu.” Maana yake si kubatiza tu, bali ni “kuzamisha” au “kujizamisha”, yaani kujizamisha au kujiingiza, kujitosa kabisa katika maisha ya kimungu, ya Mungu Baba, ya Mungu Mwana na ya Mungu Roho Mtakatifu. Kazi waliyokabidhiwa wafuasi inaendelea kwetu hata katika udhaifu wetu ni ile ya kuwazamisha wengine na ya kujizamisha wenyewe katika maisha ya Mungu, maisha ya upendo. Kazi hiyo amekabidhiwa kila mwamini.


Kisha inakuja sasa hatima nzuri tunayosherehekea leo, kwamba “mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.” Kupaa si kuachana na mfufuka, bali yuko pamoja nasi hata kama mahasa yetu hayawezi tena kumwona na kumshika. Leo yuko nasi, yuko karibu zaidi nasi katika kazi yetu hii ya kujenga ulimwengu katika maisha ya utatu na ya upendo. Kama hatima ya Yesu ni hiyo, basi tunayo sababu ya kusherekea kupaa kwake, kwani amaeyapaisha maisha yetu juu mlimani. Tunaweza pia kuusherekea msiba.

“Usihangaike usione hofu,
yote yanapita Mungu hageuki,
utapata yote kwa saburi ukipenda kumshiriki Yeye,
Mungu peke yake anatosha.”

Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.