Mshikamano, amani na matumaini kwa Sudan ya Kusini!
Shirikisho la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kimissionari ya Kanisa Katoliki yanayotekeleza
utume wake nchini Sudan ya Kusini yamewaandikia waamini na watu wote wenye mapenzi
mema ujumbe wa mshikamano, amani na matumaini wananchi wote wa Sudan ya Kusini katika
kipindi hiki kigumu cha historia ya nchi yao; kipindi ambacho mtutu wa bunduki unaonekana
kutawala zaidi kuliko majadiliano yanayolenga upatikanaji wa amani ya kudumu!
Kuna
Mashirika ya Kitawa 29 yanayojikita katika Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji
ya mtu mzima: kiroho na kimwili nchini Sudan ya Kusini. Mashirimka haya yanasema yataendelea
kuwahudumia wananchi wa Sudan ya Kusini kama sehemu ya utekelezaji wa mchakato wa
Uinjilishaji kwa kutoa huduma katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu katika
majimbo saba yanayounda Kanisa Katoliki Sudan ya Kusini.
Mashirika haya yanapenda
kuonesha mshikamano wake wa dhati na upendo kwa wananchi wa Sudan ya Kusini kwa kuthamini
utu na heshima ya kila mtu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, ili kujenga na kuimarisha:
umoja, upendo na mshikamano wa dhati kati ya watu. Wanasikitishwa sana kutokana na
vitendo vya umwagaji wa damu ya watu wasiokuwa na hatia vinavyoendelea kwa wakati
huu nchini Sudan ya Kusini.
Maelfu ya wananchi wa Sudan ya Kusini wanatamani
kuona tena haki, amani, upendo na mshikamano vikitawala miongoni mwao. Watawa wa Mashirika
haya wanasema, mawazo yao wanayaelekeza zaidi kwa familia ambazo zimeguswa kwa namna
ya pekee na machafuko ya kisiasa nchini Sudan ya Kusini. Wanatambua kwamba, kuna maelfu
ya watu ambao wamelazimika kuyakimbia makazi yao kwa kuhofia usalama wa maisha na
mali zao; ni watu ambao wamekimbilia msituni au kwenye kambi za wakimbizi za Umoja
wa Mataifa.
Wanapenda kuonesha mshikamano wao kwa Makleri na Watawa walionyanyasika
kutokana na machafuko haya ambayo yanaendelea kusababisha uharibifu mkubwa kwa miundo
mbinu ya nyumba za ibada, shule, hospitali na makazi ya watu. Watawa wa Mashirika
haya wanawapongeza wote ambao wameendelea kuonesha mshikamano wa dhati na watu wanaoteseka
kutokana na machafuko ya kisiasa pamoja na vita nchini Sudan ya Kusini.
Mashirika
ya kitawa na kazi za kitume nchini Sudan ya Kusini yanalaani vita na mauaji ya watu
wasiokuwa na hatia yanayofanywa na Serikali pamoja na wapinzani wake. Kumekuwepo na
uvunjifu mkubwa wa haki msingi za binadamu, wizi na uporaji wa mali ya umma na binafsi,
lakini katika yote haya wahusika wakuu katika machafuko yanayoendelea Sudan ya Kusini
watambue kwamba, utu na heshima ya binadamu ni mambo yanayopaswa kulindwa, kutetewa
na kuendelezwa.
Mashirika ya kitawa yanalaani tabia ya rushwa, wizi na ufisadi
wa mali ya umma; ukabila; chuki na uhasama; uchu na uroho wa madaraka mambo ambayo
yamechangia umwagaji wa damu ya watu wasiokuwa na hatia. Hata katika mazingira ya
mauaji na uvunjifu wa haki msingi za binadamu, kuna watu wanaoendelea kutajirika kutokana
na uwepo wa biashara haramu ya silaha inayochochea vita na machafuko ya kijamii, hivi
ni vitendo vya kinyama ambavyo kamwe haviwezi kufumbiwa macho!
Mashirika ya
kitawa na kazi za kitume yanasema kwamba, yataendelea kushirikiana na Kanisa mahalia
katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na
kimwili kwa kushirikiana na watu wote wenye mapenzi mema katika harakati za kuponya
madonda ya vita, chuki na kinzani nchini Sudan ya Kusini, ili haki, amani, upendo
na mshikamano wa kitaifa viweze kutawala tena.
Mwishoni, Mashirika haya yanasema,
yataendelea kuwahudumia wananchi wa Sudan ya Kusini kwa ari na moyo mkuu, kwa kujikita
katika moyo wa mshikamano, furaha na matumaini kwa ajili ya leo na kesho iliyo bora
zaidi kwa wananchi wa Sudan ya Kusini.