2014-05-30 11:54:16

Wanasiasa onesheni ukweli, uwazi na uaminifu kwa umma!


Askofu Felix Ajakaye wa Jimbo Katoliki Ekiti, Nigeria katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 10 tangu Kanisa la Parokia ya Fumbo la Utatu Mtakatifu lilipozinduliwa katika Jimbo kuu la Abuja, amewataka Wakristo walioko kwenye uwanja wa kisiasa kushiriki kikamilifu kwa kuonesha uaminifu na uwajibikaji katika kulinda na kutetea mafao ya wengi, ustawi na maendeleo ya wananchi wote wa Nigeria.

Ushuhuda wa maisha unapaswa kujionesha katika medani mbali mbali za maisha na kwa njia hii wanashiriki kwa dhati kabisa katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu, changamoto kubwa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo na kwa namna ya pekee nchini Nigeria. Wakristo wajipambanue kwa huduma makini, uadilifu, ukweli na uwazi katika kuwahudumia wananchi wa Nigeria, ili kweli waweze kuwa ni mfano bora wa kuigwa na jirani zao wengine.

Askofu Felix Ajakaye anasema, huu ndio ushuhuda wa imani katika matendo, inayoonesha mashiko na mvuto kwa wananchi mbali mbali kwani watu wamechoka na maneno matupu yanayotolewa kwa kiasi kikubwa na wanasiasa. Kwa bahati mbata tasnia ya siasa imeingiliwa na watu wenye uchu wa mali, madaraka na sifa, kiasi cha kuwafanya watu wengi kuchukia mambo ya kisiasa kwani wanaona siasa kuwa ni mchezo mchafu!

Hii inatokana na ukweli kwamba, kuna watu wanavamia jukwaa la kisiasa kwa kutaka kujitajirisha wao na familia zao badala ya kuwa ni huduma makini kwa jamii. Kutokana na dhana kama hii, Kanisa halina budi kusimama kidete kuwaelimisha watu kuzingatia utawala bora; ukweli na uwazi; ustawi na maendeleo ya wengi. Wanasiasa wajenge utamaduni wa kuwa watu wanaosimamia na kutetea ukweli na uaminifu.

Ushuhuda huu unapaswa kuonekana kwa namna ya pekee miongoni mwa wanasiasa Wakristo wanaoshirikisha karama na mapaji waliyokirimiwa na Roho Mtakatifu kwa ajili ya wote. Askofu Felix Ajakaye anasema kuna haja kwa wanasiasa kujielekeza zaidi na zaidi katika ukweli, uaminifu na uwajibikaji makini kwa watu wao.







All the contents on this site are copyrighted ©.