2014-05-30 06:55:06

Siku kuu ya Kupaa Bwana Mbinguni


Ninakuleteni tena tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, leo tukiwa tunasherehekea Sikukuu ya KUPAA BWANA MBINGUNI. Sikukuu hii huja siku kumi kabla ya Pentekoste yaani siku 40 baada ya Ufufuko wa Bwana, wakati Mitume wakimsubiria Roho Mtakatifu.

Baada ya kazi ya kichungaji na kimisionari hapa duniani Bwana lazima akatoe taarifa kwa Baba yake wa mbinguni. Kumbe, anapaa mbinguni kwenda pia kutayarisha makao kwa ajili yetu sote.

Mpendwa msikilizaji, kupaa ni kuingia katika utukufu wa Mungu na kuachana na kifungo cha kifo. Ni kutenganisha dunia yetu na Mungu na hasa ni kuwa karibu na Mungu. Aidha Bwana kabla ya kupaa ataweka wazi wajibu kwa Mitume na jumuiya ya kwanza, akisema “nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.

Basi enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi. Akitambua kwamba wanahitaji msaada wake daima anawapa tumaini na kuwahakikishia akisema, na tazama nipo pamoja nanyi siku zote hata ukamilifu wa dahari” Ujumbe huu tunaupata katika Injili ya Matayo sura ya 28.

Kristo anapopaa anaingia katika utukufu wa Mungu, ni utukufu ambao hatuwezi kuugusa bali kwa njia ya imani tunaweza kuufikia. Hata hivyo Bwana kabla ya kupaa katika kipindi cha siku 40 anatoa wosia mbalimbali: Anawaambia Mitume wasitoke Yerusalemu hadi ahadi ya Baba yake itimie yaani ya kuwapelekea Roho Mtakatifu atakayewasidia katika utume wao, yaani watatenda na kubatiza katika Roho Mtakatifu. Anawaambia watapokea Roho wa Mungu na watakuwa mashahidi katika Uyahudi na Samaria yote. (Mdo 1:8).

Mpendwa ujumbe huu, si kwa ajili ya Mitume tu bali kwa ajili ya Kanisa zima, ndiyo kusema tuaalikwa kuitikia wosia wa Mungu daima ambao tunaupata kwa njia ya Neno lake na hasa kuwa mashahidi wa upendo kwa mataifa kama tulivyosikia Dominika iliyopita.

Mtume Paulo akiwaandikia Waefeso anakazia imani katika Bwana na anawakumbusha kuwa Kristu ni mfufuka na ni kichwa cha Kanisa tena ameketi kuume kwa Mungu na atawala falme zote za dunia. Aidha, anasema maisha yao hayafungwi na ulimwengu bali wanaalikwa kuishi katika tumaini la kumsubiri Kristu ajaye. Mpendwa msikilizaji, nasi tunaalikwa pia kukumbuka si watu wa ulimwengu huu bali tukishafufuliwa na Bwana tunatazama yaliyo ya juu, tunaishi pamoja na Kristu.

Mpendwa, Bwana anapopaa kuna matukio ambata yanayopaswa kutafakariwa. Kwanza kuna watu wawili wenye nguo nyeupe, hawa ni wawakilishi wa utakatifu wa Bwana, ni alama ya uwepo wa Mungu pamoja na Kristu, kumbuka pale kaburini yule aliyekuwa amekalia jiwe! Maneno waliyoyasema hawa watu wawili ni ujumbe toka kwa Mungu, yafaa na ni lazima kuushika ujumbe huo. Linatokea wingu, hili latukumbusha safari ya Waisraeli kule jangwani wakitoka Misri.

Ndiyo kusema waliongozwa na Mungu kwa njia ya wingu, na hivi wingu ni ishara ya uwepo wa Mungu (Kut.13:22). Mitume na wengine yaani watu wa Galilaya wanatazama juu na kisha ujumbe unatoka ukiwaambia vivyohivyo alivyokwenda ndivyo atakavyorudi. Kutazama juu kadiri ya wanamaandiko ni kumwelekea Mungu lakini pia watukumbusha kuhangaikia upendo hapa duniani ili kutazama kwetu juu kuwe na mzizi wa upendo uliojaa wajibu wa huduma kwa walio wahitaji.

Mpendwa msikilizaji mwinjili Matayo anatuwekea mahali pa kukutana Bwana na Mitume kuwa ni Galilaya na si Yerusalemu. Anataka tuelewe kuwa Mitume walilazimika kuanzia kazi yao ya kitume mahali Bwana alipokuwa ameanzia utume wake hadharani. Kumbukeni kuwa Galilaya haikuwa inathaminiwa na watu wa Yerusalemu, lakini Bwana anaithamini na kuipa hadhi akimaanisha kuwa mwanga ni kwa ajili ya wote.

Bwana atakutana na wanafunzi wake pale mlimani, alama ya mlima katika Injili ya Matayo ni sehemu maalum ambapo Mungu hujidhirisha. Mwinjili Matayo anaonesha jambo la ajabu kidogo lakini la maana sana akisema “baadhi ya Mitume walikuwa na mashaka”. Mbona walikukutana na Bwana mfufuka pale Yerusalemu?

Katika hili ataka kutuambia hivi leo kuwa, hakuna jumuiya iliyo kamilifu, bali mchanganyiko wa wema na wabaya. Mashaka ya Mitume ni tumaini kwetu maana katika maisha ya imani hatuna uwezo wa kutambua na kujua kila kitu, isipokuwa kujua kwamba Bwana yu pamoja nasi na ataweza kutanzua mashaka yetu.

Mpendwa msikilizaji, Bwana anapotoa wajibu kwa Mitume anaweka pia katika Mitume nguvu au mamlaka ya kutekeleza wajibu huo, ndiyo maana mwanzoni atasema nimekabidhiwa mamlaka yote na sasa nawatuma enendeni mkafanye. Mamlaka aliyopewa anawapa Mitume kwa ajili ya kutangaza habari ya wokovu, kumfanya yeye atukuke katika maisha ya watu. Mamlaka anayowapa ni ya kuwafungulia watu waingie katika Kanisa na wawe watoto wa Mungu kwa njia ya ubatizo katika UTATU MTAKATIFU.

Mpendwa mwana wa Mungu, shamrashamra za Kupaa Bwana zinaambatana na wajibu wa kuhubiri injili kwa kila kiumbe na kwa mataifa tukibatiza katika Utatu Mtakatifu. Na katika kuhubiri, mwinjili akinukuu maneno ya Bwana anatuhakikishia uwepo wa Bwana pamoja nasi mpaka ukamilifu wa dahari. Bwana anataka kututoa katika mashaka na wasiwasi unaoweza kujitokeza katika maisha ya kichungaji wakati Kanisa litakapozaliwa na kuendelea na kazi ya wokovu wa watu.

Kuwepo kwa Bwana kutokana na tangazo hili ni kiini cha furaha yetu hivi leo katika Kanisa na ulimwengu wa leo. Bwana kabla ya ufufuko alibanwa na jiografia yaani katika mazingira ya Israeli, lakini baada ya ufufuko habanwi na mazingira bali mwanga na furaha kwa mataifa yote.

Mpendwa msikilizaji, ni katika mantiki hiyo nakualika unaposhangilia Kupaa Bwana uweke nia ya pekee kwa ajili ya kazi ya kimisionari kwa njia ya sala na majitoleo mbalimbali katika familia na Kanisa kwa ujumla. Kumbuka wajibu wa kubatiza aliotuachia Bwana yaani kuwajalia watu uzima kama wajibu msingi na ufunguo mlango wa imani, kumbe kadiri ya taratibu za Kanisa la ulimwengu na Kanisa mahalia ukaushike vema na hivi Kanisa la Mungu likue na kuzaa matunda.

Mpendwa, nikutakie furaha na mapendo ukisubiri ujio wa Roho Mtakatifu Dominika ijayo. Tumsifu Yesu Kristu. Tafakari imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.