Kardinali Thèodore Adrian Sarr, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dakar Senegal, hivi karibuni
ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama kilele cha Jubilee ya miaka 150 ya Kikanisa
cha Ngasobil, kilichoko kwenye Seminari ndogo ya Mtakatifu Yosefu, Jimboni humo.
Katika mahubiri
yake, amewataka wananchi wa Senegal wanapojiandaa kwenye mchakato wa uchaguzi mkuu
unaotarajiwa kufanyika nchini humo Mwezi Juni, 2014, kuzingatia: haki msingi, utu
na heshima ya binadamu. Haya ni mambo msingi ambayo Mama Kanisa anapenda kuyakazia
kwa waamini na watu wenye mapenzi mema, ili kukuza amani, utulivu na demokrasia ya
kweli.
Haki kadiri ya Maandiko Matakatifu anasema Kardinali Sarr ni utekelezaji
wa majukumu ya mtu kadiri ya mapenzi na mpango wa Mungu kwa binadamu. Hapa matendo
yanazungumza zaidi kuliko maneno, kwani waswahili husema “maneno matupu hayavunji
mfupa”.
Kardinali Sarr amewataka wananchi wa Senegal kusimama kidete kulinda
na kudumisha utu na heshima ya binadamu hasa katika maeneo ya kazi ambako kuna hatari
ya kudhalilisha utu na heshima ya binadamu kwa kutaka kupata faida kubwa. Binadamu
ni rasilimali kazi, inayopaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa katika mchakato mzima wa
uzalishaji na utoaji huduma kwa jamii.
Ni wajibu kwa wanasiasa kuzingatia
kwamba, lengo la kazi ni kumsaidia mfanyakazi kukamilisha utu na heshima yake kama
binadamu. Amewataka wanasiasa wanaogombea nafasi mbali mbali za uongozi nchini humo
kuibua sera na mikakati inayotekelezeka, ili watakapopata ridhaa ya kuwaongoza wananchi
waweze kutekeleza kwa vitendo yale ambayo wanahidi wakati huu wa kampeni za uchaguzi,
kwa kuzingatia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.