Chama cha Kitume cha Uamsho wa Kikristo katika mkutano wake wa kitaifa uliohitimishwa
hivi karibuni, kinasema, kimepokea kwa mikono miwili taarifa za uwepo wa Baba Mtakatifu
Francisko katika Kongamano lake la Kitaifa litakaloadhimishwa hapo tarehe 1- hadi
2 Juni 2014 kwenye Uwanja wa Michezo wa Olympic, mjini Roma. Hii itakuwa ni
Siku kuu ya Kupaa Bwana Mbinguni kwa Mwaka 2014. Kongamano hili litaongozwa na kauli
mbiu “Tubuni! Aminini! Mtampokea Roho Mtakatifu. Kwa ajili ya Kanisa katika mwelekeo
wa Kimissionari”.
Chama cha Kitume cha Uamsho wa Kikristo; waamini na watu
wote wenye mapenzi mema, wameanza kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya Maadhimisho ya
Tukio hili la kihistoria linalojipambanua kwa kuwa ni fursa ya Sala na Uinjilishaji,
kama sehemu ya utekelezaji wa mchakato wa changamoto zinazoendelea kutolewa na Baba
Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wa Kanisa. Wakristo wanahimizwa kutoka
huko “walikojificha” ili kutangaza, kushuhudia na kuwaonjesha jirani zao Injili ya
Furaha.
Uwepo wa Baba Mtakatifu katika kongamano hili ni tukio la kihistoria
kwa Chama cha Kitume cha Uamsho, kinachoonesha utashi na jitihada za Chama hiki kutaka
kuunga mkono juhudi na mikakati ya kichungaji inayoendelea kuainishwa na Baba Mtakatifu
Francisko katika maisha na utume wa Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu
ya Ukristo. Kanisa halina budi kujikita katika huduma kwa walimwengu.
Kwa mara
ya kwanza Papa Francisko ataingia kwenye Uwanja wa michezo wa Olympic ulioko Roma,
ili kukutana na kuzungumza na wanachama wa Uhamsho wa Kikristo wapatao 50, 000 kutoka
ndani na nje ya Italia. Ni kongamano ambalo litawashirisha baadhi ya viongozi waandamizi
kutoka Vatican na wanachama mashuhuri wa chama cha Uhamsho kutoka sehemu mbali mbali
za dunia.
Akizungumzia kuhusu tukio hili, Bwana Salvatore Martinez, Rais wa
Chama cha Kitume cha Uamsho wa Kikristo anapenda kumshukuru Baba Mtakatifu Francisko
kwa kukubali mwaliko wao na kuamua kushiriki. Waraka wa kichungaji wa Baba Mtakatifu
Francisko: Injili ya Furaha, waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee kuonja ile Injili
ya Furaha inayobubujika kutoka kwa Yesu Kristo; kutambua na kung’amua utamu na uzuri
wa kusali kama Jumuiya; kusikia ile nguvu ya ndani inayowasukuma waamini kujitosa
kifua mbele ili kutangaza na kushuhudia Ibada ya Kuabudu, Sala ya Shukrani na Kusifu
na neema ya Mungu inavyotenda kazi kwa Watu wa Mungu.
Bwana Salvatore anasema
haya ni mambo msingi yanayowapambanua wanachama wa Chama cha Uamsho wa Kikristo katika
maisha na utume wao ndani ya Kanisa Katoliki; chama ambacho kwa sasa kinatimiza miaka
45 tangu kilipoanzishwa. Baba Mtakatifu Francisko anawafahamu fika kwani alikuwa ni
mlezi wa Chama hiki alipokuwa bado nchini Argentina.
Hiki ni kipindi cha Uinjilishaji
Mpya, mwaliko kwa waamini kutoka kifua mbele, kumshuhudia Kristo katika uhalisia wa
maisha yao! Huu utakuwa ni mwanzo tu, lakini shughuli yenyewe itafanyika rasmi wakati
wa Mkesha wa Siku kuu ya Petentekoste, Siku ya kuzaliwa kwa Kanisa, Siku ya Waamini
Walei ndani ya Kanisa.