2014-05-29 08:20:58

Ogopa Mashahidi wa Uganda!


Askofu Paul Ssemwogerere wa Jimbo Katoliki la Kasana-Luweero, Uganda, hivi karibuni ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu katika Madhabahu ya Mnyonyo yaliyoko nje kidogo ya Jimbo kuu la Kampala kwa kusema kwamba, Mashahidi wa Uganda wamesaidia kwa kiasi kikubwa kuipatia Uganda heshima kubwa katika Jumuiya ya Kimataifa.

Watu wengi wanaikumbuka Uganda kutokana na mauaji ya Idd Amin Dada, rushwa na ufisadi, Ukimwi na vita ya wenyewe kwa wenyewe inayoendeshwa na Jeshi la Waasi wa Uganda kwa kipindi cha miaka kadhaa sasa! Matukio yote haya yanaipaka matope Uganda licha ya mambo mazuri yanayoendelea kufanyika nchini humo.

Askofu Ssemwogerere ameyasema hayo wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu katika eneo ambalo Mashahidi wa Uganda walianzia safari ya ujasiri wa imani, uliowapeleka hadi katika Namugongo ili kukabiliana na kifo kutokana na imani thabiti kwa Kristo na Kanisa lake. Waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia kila mwaka wanamiminika nchini Uganda kutembelea mahali ambapo Mashahidi wa Uganda waliyamimina maisha yao bila ya kujibakiza kama kielelezo cha uaminifu kwa Kristo, utu na maadili mema!

Askofu Ssemwogerere anasema, kuna baadhi ya wazazi ambao wamesahau na kutelekeza wajibu wao katika familia, jambo ambalo linagumisha malezi na makuzi ya watoto na vijana ndani ya Jamii. Wazazi wanakosa muda wa kuwafunda watoto wao katika maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili kwani wametingwa mno na malimwengu, lakini madhara yake ni makubwa kwa ustawi na maendeleo ya jamii. Wazazi hawana muda wa kusali wala kwenda Kanisa pamoja na watoto wao! Hapa ni hatari kwa malezi ya kiroho, kumbe kuna haja kwa wazazi kutekeleza wajibu wao barabara bila kutega!

Athari za utandawazi na maendeleo ya teknolojia zinawafanya baadhi ya wazazi na walezi kushindwa kujiheshimu mbele ya watoto wao, dalili za kumong'onyoka kwa maadili na utu wema! Askofu Ssemwogerere anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema nchini Uganda kuwaomba Mashahidi wa Uganda kuwaombea ili waweze kutekeleza wajibu wao barabara ndani ya familia na jamii katika ujumla wake, ili kweli waweze kuwa ni mfano bora wa maadili na utu wema.

Mashahidi wa Uganda waliuwawa kikatili kunako tarehe 26 Mei 1886. Lakini, Kanisa linawakumbuka rasmi kila mwaka ifikapo tarehe 3 Juni. Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Andrea Kaggwa na Dennis Ssebuggwaawo waliuwawa kikatiliki na Kabaka Mwanga katika eneo la Munyonyo, Kampala, Uganda. Kanisa Katoliki nchini Uganda lilimteua Mtakatifu Andrea Kaggwa kuwa Msimamizi wa Makatekista, waalimu wa shule na familia.

Baada ya kuuwawa kikatili na Kabaka Mwanga, Wakristo waligeuza nyumba ya Kaggwa kuwa ni Kikanisa mahali ambapo waliweza kukusanyika ili kupata mafundisho ya Katekesi. Damu ya Mashahidi wa Uganda iwe ni kikolezo cha imani, matumaini, mapendo, maadili na utu wema. Familia zijitahidi kutekeleza dhamana na wajibu wao!







All the contents on this site are copyrighted ©.