2014-05-29 08:40:56

Maaskofu wataka Wamissionari waliotekwa nyara kuachiliwa huru!


Baraza la Maaskofu Katoliki Cameroon linakitaka Kikundi cha Boko Haram kilichowateka Mapadre wawili na mtawa mmoja kuwaachilia mara moja ili waweze kuendelea na utume wao miongoni mwa wananchi wa Cameroon. Itakumbukwa kwamba, Wamissionari hawa walitekwa nyara nchini Cameroon hapo tarehe 5 Aprili 2014 na hadi sasa hawajulikani mahali walipo!

Ombo hili limetolewa hivi karibuni na Kardinali Christian Tumi, Askofu mstaafu wa Jimbo kuu la Doula nchini Cameroon. Kikundi cha kigaidi cha Boko Haram kinausishwa na vitendo vya utekaji wa watu nyara, Kaskazini mwa Afrika. Wakati ambapo Jumuiya ya Kimataifa inasema hakuna sababu ya kufanya majadiliano ya magaidi wa Boko Haram bali ni kuendelea kula nao sahani moja hadi kieleweke, lakini baadhi ya viongozi wa Serikali ya Cameroon kama ilivyokuwa hata Nchini Nigeria wanasema, kuna haja ya kufanya majadiliano, ili mateka waweze kuachiliwa huru na pia kudumisha utulivu.

Rais Paul Biya wa Cameroon, hivi karibuni alipokuwa anashiriki mkutano dhidi ya vitendo vya Boko Haram Kaskazini mwa Afrika, uliokuwa umeitishwa na Rais Francois Hollande wa Ufaransa alitangaza vita dhidi ya vitendo vya kigaidi nchini mwake. Kanisa nchini Cameroon linasema nguvu yake inajikita katika majadiliano kwani hawana silaha ya kupambana na magaidi. Hii ni changamoto kwa Serikali kujikita katika utekelezaji wa mikakati endelevu ya ulinzi na usalama wa raia na mali zao!







All the contents on this site are copyrighted ©.