2014-05-28 11:43:40

Taarifa ya kazi duniani kwa Mwaka 2014


Taarifa ya Shirika la Kazi Duniani, ILO kwa Mwaka 2014 inaonesha kwamba, katika kipindi cha miaka mitano ijayo, watu millioni 213 wataingia katika soko la ajira duniani na kati yao kuna watu millioni mia mbili ni wale wanaotoka katika Nchi zinazoendelea duniani.

Hapa kuna changamoto kubwa ya kuhakikisha kwamba, kunafanyika maboresho katika maeneo ya kazi pamoja na kuwapatia wafanyakazi maisha bora zaidi. Katika nchi zinazoibukia kwenye masuala ya kiuchumi kuna zaidi ya watu millioni 839 walioajiriwa lakini wanaishi kwa dolla moja ya kimarekani kwa siku!

Shirika la Kazi Duniani katika taarifa yake inayoangalia uchumi wa Nchi zinazoendelea duniani inaonesha kwamba, kuna idadi kubwa ya vijana ambao hawana fursa ya ajira kwa asilimia 12% ikilinganishwa na watu wazima. Afrika ya Kaskazini na Mashariki ya kati ni kati ya maeneo ambayo yamekumbwa kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa fursa za ajira duniani, kwani takwimu zinaonesha kwamba, kati ya vijana watatu mmoja hana fursa ya kupata ajira.

Kwa bahati mbaya wasichana wameathirika zaidi, kwani wasichana wasiokuwa na ajira katika eneo hili ni asilimia 45%. Shirika la Kazi Duniani linasema kwamba, maboresho katika ubora wa kazi unaweza kusaidia kupungua tofauti kubwa za fursa za ajira zinazojitokeza kwa sasa.

Sheria za kazi hazina budi kuzingatiwa pamoja na kuendelea kuunga mkono sera zinazosaidia kutengeneza fursa za ajira pamoja na kuwapatia wafanyakazi maisha bora zaidi kama motisha katika uzalishaji na tija anasema Guy Ryder, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Kazi Duniani. Fursa bora za ajira ni nyenzo muhimu sana katika mapambano dhidi ya umaskini duniani. Kiwango cha chini cha mshahara ni jambo ambalo limeendelea kupiganiwa na wafanyakazi sehemu mbali mbali duniani ili kuondokana na ubaguzi unaofanywa hata katika viwango vya mshahara.

Shirika la Kazi Duniani linasema, kuna haja kwa Nchi changa duniani kujifunga kibwebwe kupambana kufa na kupona na kazi za suluba zinazowaingizia wahusika faida ya kiasi cha dolla za kimarekani millioni 150, lakini inaacha madonda makubwa katika maisha ya wafanyakazi na familia zao. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya watu millioni 21 wanaofanya kazi za suluba sehemu mbali mbali duniani. Hapa wasichana na wanawake wanaotumbukizwa kwenye biashara haramu ya ngono ambayo faida yake inakadiriwa kufikia dolla billioni 99. Udhalilishaji wa kijinsia ni kati ya changamoto kubwa kwenye sekta ya kazi na ajira duniani. Dhuluma hii inawakumba hata watu wanaofanya kazi majumbani, kwenye sekta ya kilimo na uvuvi.

Shirika la Kazi Duniani linaonesha kwamba, Bara la Asia linaongoza kwa biashara ya ngono duniani kwa kuwa na watu zaidi ya millioni kumi na mbili, lakini pia linaongoza kwa kupata faida kubwa katika masuala ya uchumi kwa kuwa na kiasi cha dolla za kimarekani billioni 52 za Kimarekani kwa mwaka. Takwimu zinaonesha kwamba, faida kwa watu binafsi kutoka katika Nchi zilizoendelea zaidi duniani ni sawa na dolla za kimarekani 35, 000 kwa kila mtu!







All the contents on this site are copyrighted ©.