Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anasema kwamba, kilele cha hija ya
kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko Nchi Takatifu, iliyokuwa inaongozwa na kauli
mbiu “Wote wawe wamoja” ilifikia kilele chake pale Patriaki Bartolomeo wa kwanza alipokutana
na kusali na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Kaburi Takatifu, kielelezo cha mwanzo
mpya wa mchakato wa majadiliano ya kiekumene kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la
Kiorthodox.
Kardinali Parolin anasema, maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili
wa Vatican sanjari na ujasiri ulioneshwa na Mtumishi wa Mungu Papa Paulo VI kwa kukutana
na Patriaki Anathegoras wa Yerusalemu ni matukio ambayo yameliwezesha Kanisa kujichunguza
na kuanza hija mpya ya maisha ya kiekumene inayojikita katika imani, upendo na ukweli,
ili wote wawe wamoja kadiri ya mapenzi ya Kristo kwa Kanisa lake. Mkutano wa viongozi
hawa wawili ni chachu kwa Kanisa zima kusonga mbele kwa ari kubwa zaidi katika mchakato
wa majadiliano ya kiekumene.
Kardinali Pietro Parolin anakiri kwamba, sala
ina nguvu ya kuweza kuleta mabadiliko katika maisha na utume wa Kanisa. Licha ya fursa,
matatizo na changamoto za kisiasa na kidiplomasia, lakini katika hija ya kichungaji
ya Baba Mtakatifu Francisko katika Nchi Takatifu, wamegundua nguvu ya sala katika
maisha na utume wa Kanisa. Kwa njia ya nguvu ya sala, viongozi wa Kanisa wanaweza
kufanya maamuzi magumu katika maisha na utume wa Kanisa. Kila upande ukipania, amani,
umoja na mshikamano vinaweza kupatikana!
Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu
wa Vatican anakumbusha kwamba, amani ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomwajibisha
binadamu. Zawadi hii ina nguvu ya kuleta mabadiliko makubwa katika maisha na mioyo
ya binadamu, kiasi cha kuwafanya kuwa kweli ni vyombo na wajenzi wa amani. Changamoto
kubwa kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema ni kuipokea zawadi hii na kuimwilisha
katika uhalisia wa maisha ya mwandamu, kwa kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze
kuleta mabadiliko ya kweli katika maisha ya mwanadamu!