2014-05-27 11:31:02

Ujenzi wa amani,hudai zaidi ya yote, kuheshimu utu wa mtu na uhuru wa kila binadamu


Baba Mtakatifu Jumatatu akiwa katika Hija ya kutembelea maeneo Matakatifu Jerusalem , pia alimtembelea Rais wa Israel, Mheshimiwa Rais Shimon Peres. Katika tukio hili, Papa alipewa zawadi na watoto wawili na pia kuweka sahihi yake katika kitabu cha wageni kilichopambwa kwa rangi ya dhahabu na kuwa na muda wa kubadilishana zawadi ukumbini na kujadiliana hoja kadhaa mbele ya ujumbe kutoka pande zote mbili, Papa akiwa ameandamana na Kardinali Pietro Parolin , Kardinali Sadri , Kardinali Tauran na Kardinali Kurt Koch , pia Patriaki Twal na , Bruda Pizzaballa.
Katika hotuba yake, Papa Francisko , alimshukuru Rais Peres kwa mapokezi na ukarimu wake. Na kuonyesha furaha ya kukutana nae tena mjini Jerusalem , mji wenye kutunza Maeneo Mtakatifu, mji mpendwa wa wafuasi wa imani kuu tatu za kidini, wanao mwabudu Mungu mmoja aliyemwita Ibrahimu . Na kwamba, maeneo Mtakatifu sio tu kuwa na makaburi au makumbusho kwa ajili ya watalii , lakini mahali ambapo jumuiya za waamini kila siku hupata kielelezo cha imani na utamaduni wao , na kutekeleza kazi yao ya upendo. Hasa kwa sababu hii , tabia yake ya utakatifu ni lazima daima iimarishwe, kwa ajili ya urithi wa tangu kale si kwa manufaa ya kizazi chetu tu lakini pia kwa vizazi vingine vijavyo. Inawezekana Yerusalemu kuwa kweli mji wa amani !

Papa alisihi iwepo nia ya kudumisha utambulisho wake na tabia yake takatifu ya kidini na utamaduni, kama jambo muhimu na kama hazina kwa ajili ya watu wote! Na kwa jinsi gani mahujaji na wakazi wanavyoweza kufurahia kuzuru Maeneo Mtakatifu bure na kwa hiari kushiriki katika sherehe za kidini.

Papa aliendelea na hotuba yake akimtaja Mheshimiwa Rais Peres kuwa mtu anayejulikana kwa fadhila zake za kuwa mtu wa amani na mpatanishi . Na alimstaajabia kwa mbinu ambazo hujichukua kwa ajili ya kulinda amani, kwanza, kwa kudai heshima kwa utu wa mtu na uhuru wa kila mtu , ambavyo Wayahudi, Wakristo na Waislamu wana imani sawa kwamba kila binadamu ameumbwa na Mungu na wana matazamio ya uzima wa milele. Hii imani ya kufanana, huwawezesha kujenga uthabiti wa kusimamia imara hoja hiyo , kuwa ndiyo njia ya ufumbuzi wa amani katika kila hila na kila utata na migogoro. Na hapo alitoa upya ombi lake kwa vyama vyote, kuepuka kila hila na kishawishi cha kutenda kinyume namamuzi ya kuwa na amani, bali wakumbatie maamuzi yenye makubaliano ya kweli, kufanya kazi bila kuchoka kwa ajili ya amani, mshikamano na umoja.
Papa alisema, kuna pia haja kwa Taasisi na vyama vya kijamii, kukataa yote yaliyo kinyume amani na mahusiano ya kuheshimiana kati ya Wayahudi, Wakristo na Waislamu, na kujiepusha na shari za kukimbilia vurugu na ugaidi, na kukataa kila aina ya ubaguzi kwa misingi ya rangi au dini , na majaribio ya kulazimisha wengine imani za kidini, kwa gharama ya haki za wengine, au dalili za kutovumilia kuelekezwa dhidi ya watu binafsi au maeneo ya kuabudu, kwa kuwa wao ni Wayahudi au Wakristo au Waislamu.
Papa alieleza na kuomba kwamba, jamii ya Kikristo ya Israel iweze kuishi na kufanya kazi katika Serikali ya Israeli, wakiwa kama sehemu ya jamii ya Israel wenye haki kamili ya kushiriki kikamilifu katika mambo ya uraia , kisiasa na kiutamaduni. Wakristo wana haki ya kuchangia na kushiriki katika utendaji wote kwa manufaa ya wote na ukuaji wa amani ; wanataka kufanya hivyo kama raia kamili wenye nia ya kukuza maridhiano na maelewano. Na alimthibitishia Rais Peres kwamba, humkumbuka katika sala na yeye Rais na watu wa Israel kwa ujumla. Na pia anawaombea wote wale wanao kabiliwa na mateso mbalimbali kwa sababu za ukatili wa kibinadamu. Amani iwe kwa taifa la Israel na Mashariki yote ya Kati. Shalom!
Kwa ajili ya kumbukumbu ya kukutana kwao, Papa Francisko na Rais Shimon Peres, kwa pamoja walipanda mti wa mzeituni, katika bustani za Ikulu Jerusalem.









All the contents on this site are copyrighted ©.