2014-05-27 07:54:29

Teknolojia ya kielektroniki na uchafuzi wa mazingira!


Ghana ni kati ya nchi za Kiafrika ambazo zimeathirika kwa kiasi kikubwa na uchafuzi wa mazingira unaotokana na mabaki ya teknolojia ya kielektroniki. Kuna marundo makubwa ya computer na vifaa vyake, majokofu, luninga, radio, majiko na pasi ambayo yamezagaa mjini Accra, Ghana. Taarifa zinaonesha kwamba, kila mwaka Ghana inaingiza tani zaidi ya 215, 000 za bidhaa ya kielektroniki ambazo tayari zimekwisha tumika kutoka Ulaya.

Ghana kwa upande wake, kila mwaka inazalisha kiasi cha tani 129, 000 za taka za kielektroniki kila mwaka. Wizara ya viwanda na biashara ya Ghana inakadiria kwamba, uzalishaji wa taka hizi utaongezeka maradufu ifikapo mwaka 2020. Marundo ya taka za kielekroniki ni matokeo ya biasha za magendo zinazofanywa na baadhi ya wananchi wasiokuwa waaminifu na matokeo yake, wameingiza hata taka zenye sumu, jambo ambalo ni hatari kwa mazingira na afya ya wananchi wa Ghana.

Watu wengi wamekuwa wakitafuta wakati mwingine riziki ya maisha yao ya siku kutoka kwenye mashimo ya taka, jambo ambalo ni hatari, kwani wakati mwingine wameunguza taka hizi kwa moto na hivyo kuendeleza uchafuzi wa mazingira. Wakati wa mvua, maji yanayotiririka kutoka katika taka hizi yanaingia mitoni na kutumiwa na watu wa kawaida.

Benki ya Dunia imeona hatari hii na kutoa onyo kwa Jumuiya ya Kimataifa kuisaidia Ghana kupambana na uchafuzi mkubwa wa mazingira, vinginevyo watu wake wengi wako hatarini kukumbwa na magonjwa mbali mbali. Wafanyabiashara wawe makini na bidhaa wanazoagiza, ili kulinda mazingira, kwani kwa uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka, Bara la Afrika linaweza kugeuzwa kuwa ni shimo la taka za teknolojia ya kielektroniki, wakati huu watu wengi wanapotaka kutumia vyombo hivi!







All the contents on this site are copyrighted ©.