2014-05-27 08:53:32

Papa akamilisha Hija yake Mashariki ya Kati na wito wa amani


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu jioni alikamilisha hija yake Mashariki ya Kati na wito wa amani. Hija hii ya siku ya tatu 24-26 Mei 2014 kutembelea maneneo Matakatifu katika Nchi Takatifu aliikamilisha, akiwa mjini Jerusalem ambako hatua ya mwisho aliongoza Ibada ya Misa akiwa na Maaskofu wa Nchi Takatifu, katika jengo lenye Chumba cha Juu ambako Kristo, alifanya karamu ya mwisho, kinachojulikana kama “cenacolo”.

Baada ya Ibada, alielekea uwanja wa ndege wa Monte Scopes , ambako alipanda helkoputa hadi uwanja wa Ndege wa Ben Gourion wa mjini Tel Aviv, ambako aliagana na wenyeji wake, viongozi wa kanisa na serikali wakiongozwa na Rais wa Israel, Shimon Peres. Mahali hapo Papa pia kulifanyika gwaride la heshima la wanajeshi. Na kabla ya kupanda ndege alitoa salaam zake za mwisho kwa wote.

Wachambuzi wa ziara hii wanasema , Jumatatu aliikamilisha Hija kwa kitendo cha ishara na wito wa amani kati ya Israel na Wapalestina na urafiki kati ya Wayahudi na Waislamu katika nchi aliko zaliwa Yesu.

Siku ya Jumapili , Papa alisikiliza kwa makini ombi la Palestina,linalo tafuta kuondolewa kwa kizuizi cha usalama kati mji wa Bethlehemu , na nchi jirani ya Israel, wanalolalamikia kwamba, kinaleta mahangaiko na kudumaza uchumi wa Palestina. Aidha kwa Upande wa Israel , Papa Francisko , alionyesha heshima zake kwa waathirika wa mauaji ya kinyama dhidi ya Wayahudi yaliyofanyika wakati wa Vita Kuu vya dunia , kwa kubusu mikono ya waathirika kadhaa, akisema kamwe unyama huo usifanyike mahali popote duniani, na alipokea ombi la Israeli la kuwakumbuka na kuwaombea, waathirika wa mabomu ya kujitoa mhanga na mashambulizi mengine .

Kati ya matukio yaliyokuwa ya kuvutia na kugusa, ni pale Papa aliposalimiana kwa kukumbatiana na Viongozi wa Kiislamu na Marabbi , na jinsi alivyo tolea sala yake katika ukuta wa Magharibi, ambako aliacha kikaratasi katika ufa, kilichoandikwa kwa mkono wake mwenyewe ombi la sala kwa “ Baba yetu '' sala ambayo ameiandika katika lugha ya Kihispaniola ambayo ni lugha yake ya asili.

Padre Federico Lombardi , Msemaji wa Vatican , ametaja mahusiano haya ya Papa na waamini wa dini zingine, kuwa jibu halisi katika matatizo yanayotokeza na pia kwa matatizo ya muda mrefu sana, ni kukumbatia na kusahau tofauti hizi. Ni kusali na kuomba msaada wa Mungu, na kupendana na kuhurumiana na kisha kukumbatia. ''

Padre Lombardi amesema, Mantiki hiyo iko moyoni mwa Papa Francisko, na ndivyo alivyotoa mwaliko wake bila kutazamiwa kwa Marais wa Israel na Palestina, kuja Vatican mwezi ujao, kwa nia ya kusali kwa ajili ya kuombea amani . Mwaliko ulio sisimua, wa kifranciskani, nia alizojionyesha tangu mwanzo wa kuchanguliwa kwake kuwa Papa kwa kuchagua jina la Francisko, akipenda kufuata nyayo za amani na upendo wa Mtakatifu Francis wa Assisi . Na hivyo Papa Francisko anajisikia wajibu wa kutekeleza nia yake hiyo ya kufanikisha amani duniani.

Papa Francisko akizungumza na wanahabari akiwa njia kurejea Roma, alisisitiza kwamba, nia ya kukutana na Marais wa Israel na Palestina ni kusali wala si kufanya majadiliano au kutafuta upatanishi. Watakutana na kusali pamoja na kisha kila mmoja atarejea nyumbani, kwake. Na alisisitiza umuhimu wa kusali pamoja.








All the contents on this site are copyrighted ©.