Watoto wanastahili kupokelewa, kutunzwa na kusaidiwa!
Baba Mtakatifu Francisko akiwa mjini Bethlehemu, Jumapili tarehe 25 Mei 2014 ameadhimisha
Ibada ya Misa Takatifu katika Uwanja wa Pango la Mtoto Yesu mjini Bethlehemu, maarufu
kama "nyumba ya mkate". Baba Mtakatifu katika mahubiri yake, ametafakari kwa kina
kuhusu Fumbo la Umwilisho. Amewashukuru viongozi wa Serikali na Kanisa, familia ya
Mungu nchini Palestina pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanaojisadaka kwa ajili
ya kuhakikisha kwamba, imani, matumaini na mapendo yanaendelea kustawi na kushamiri
kati ya watu!
Yesu Kristo aliyezaliwa mjini Bethlehemu ni alama wazi kutoka
kwa Mwenyezi Mungu kwa watu waliokuwa wanasubiri wokovu. Ameendelea kuwa ni kielelezo
makini cha upole na uwepo wa Mungu duniani. Mtoto Yesu kama walivyo watoto wengine
wote duniani ni alama ya matumaini, maisha na utu. Ni kielelezo cha taifa, jamii na
dunia inayothamini tunu msingi za maisha ya familia. Mambo haya yanawezekana pale
tu, watoto wanapopokelewa, wanapopendwa, wanapolindwa na kuthaminiwa, hapo kwa hakika
familia inaweza kushamiri. Baba Mtakatifu anaipongeza taasisi ya Effeta ya Paulo VI
inayohudumia watoto viziwi kutoka Palestina!
Mtoto Yesu kama walivyo watoto
wengine wote anasema Baba Mtakatifu ni dhaifu, anahitaji kusaidiwa na kutunzwa, changamoto
ya kuwapokea na kuwalinda watoto tangu wanapotungwa mimba tumboni mwa mama zao. Lakini
inasikitisha kuona kwamba, kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, kuna watoto
wanaoishi katika mazingira hatarishi pembezoni mwa miji mikuu au vijijini. Ni watoto
wanaonyanyaswa na kudhulumiwa; wanaofanyishwa kazi za suluba au kuzamishwa maji huko
kwenye Bahari ya Mediterania. Haya yote ni matendo ya aibu sana mbele ya Mwenyezi
Mungu, aliyejifanya Mtoto.
Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini na watu
wote wenye mapenzi mema kuiga mfano wa Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu waliomlinda
na kumtunza Mtoto Yesu dhidi ya ukatili wa Herode! Waige mfano wa wachungaji kutoka
kondeni waliokwenda kumwabudu Mtoto Yesu. Kimsingi watu wajenge utamaduni wa kusikiliza,
kuwalinda na kusali kwa ajili ya watoto. Kilio cha watoto, kiashe dhamiri za watu
kuwahudumia kwa upendo, kwa kuguswa na mahitaji ya watu wanaokufa kwa njaa duniani
wakati ambako sehemu nyingine za dunia watu wanakula na kusaza. Watoto wapewe huduma
bora za tiba, kwa kuwalinda na kuondokana na biashara haramu ya silaha inayowanyanyasa
watoto kwa kuwapeleka vitani au kuwafanyisha kazi ngumu.
Baba Mtakatifu anahitimisha
mahubiri yake kwa kusema, kila mtoto anayezaliwa duniani kama ilivyokuwa kwa Mtoto
Yesu anapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na familia, jamii na ulimwengu katika ujumla
wake. Huu ni mwaliko wa kuwa na mwelekeo mpya wa maisha unaojikita katika mahusiano
mema pasi na kinzani, vita, ulaji wa kupindukia. Watu wajitahidi kujenga mahusiano
ya kidugu, kwa kusameheana, kujipatanisha pamoja na kushirikishana tone la upendo!