Baba Mtakatifu Francisko Jumapili tarehe 25 Mei 2014 baada ya maadhimisho ya Ibada
ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Pango la Mtoto Yesu mjini Bethlehemu, amesali pamoja
na waamini Sala ya Malkia wa Mbingu, mahali hapa ambapo Bikira Maria alimzaa Mtoto
Yesu, akapata nafasi ya kuutafakari uso wa Yesu kuliko mtu mwingine yoyote duniani.
Akasaidiwa na Mtakatifu Yosefu kumlaza Mtoto Yesu katika Pango la kulishia wanyama!
Baba
Mtakatifu amewaweka wananchi na wakazi wote wa eneo hili chini ya ulinzi na tunza
ya Bikira Maria, ili waweze kuishi katika haki, amani na udugu. Amewaweka pia mahujaji
wote wanaotoka sehemu mbali mbali duniani kuja mjini Bethlehemu ili kujichotea neema
kutoka kwenye kisima cha imani ya Kikristo, chini ya ulinzi wa Bikira Maria.
Baba
Mtakatifu anamwomba Bikira Maria kulinda familia, vijana na wazee; kuwasaidia wale
ambao wamepoteza imani na matumaini; awafariji wagonjwa, wafungwa na wote wanaoteseka;
awaimarishe viongozi wa dini na Jumuiya nzima ya waamini, ili kweli waweze kuwa ni
chumvi na mwanga wa katika Nchi hii. Baba Mtakatifu anamwomba Bikira Maria alinde
huduma za elimu zinazotolewa katika eneo hili, lakini zaidi kutoka Chuo Kikuu cha
Bethlehemu.
Baba Mtakatifu anapotafakari kuhusu Familia Takatifu, mawazo yake
yanakwenda moja kwa moja mjini Nazaret ambako anatamani kwenda kutembelea Mwenyezi
Mungu akipenda wakati mwingine tena. Ameonesha upendo na mshikamano wake kwa waamini
wote wanaoishi katika eneo hili. Anamwomba Bikira Maria asaidie mchakato wa ujenzi
wa udugu, mshikamano na amani!