Biashara haramu ya silaha ni chanzo cha vita na mahangaiko ya watu!
Baba Mtakatifu Francisko baada ya kuwasili nchini Yordani, akapata nafasi ya kuzungumza
na wenyeji wake, akaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Michezo wa Kimataifa
mjini Amman, jioni alitembelea eneo la Bethania ng'ambo ya mto Yordan, mahali alipobatizwa
Yesu. Hapo alipata nafasi ya kusali kwa ukimya.
Baadaye, Baba Mtakatifu Francisko
alikutana na wakimbizi pamoja na vijana walemavu, kwenye Kanisa ambalo Baba Mtakatifu
mstaafu Benedikto XVI aliweka jiwe lake la msingi kunako mwaka 2009. Baba Mtakatifu
alipata nafasi ya kusikiliza shuhuda mbali mbali zilizotolewa na wakimbizi pamoja
na walemavu hao!
Baba Mtakatifu katika hotuba yake amesema, kwa makusudi kabisa
aliamua kukutana nao ili kuweza kuuona uso wa Yesu Msulubiwa na upendo wake unaowakirimia
wanadamu utu na wokovu. Baba Mtakatifu amewashukuru viongozi wa Serikali nchini Yordan,
wananchi na Mashirika ya misaada ya Kanisa Katoliki yanayotekeleza utume wake miongoni
mwa wakimbizi bila ubaguzi. Hiki ni kielelezo cha huruma ya Yesu.
Baba Mtakatifu
kwa mara nyingine tena anaiomba Jumuiya ya Kimataifa kusaidia mchakato wa kuleta amani
na upatanisho wa kitaifa nchini Syria. Anawahimiza vijana kujitosa kimasomaso kushiriki
katika ujenzi wa jamii inayojikita katika msingi wa haki na heshima kwa maskini! Watu
wanapenda amani, lakini bado kuna watu wanaotaka kujitajirisha kwa kuchochea chuki,
ghasia na vita ili kukuza soko la biashara haramu ya silaha. Baba Mtakatifu anawaalika
wote wanaojihusisha na biashara haramu ya silaha, kutubu na kuongoka, ili kweli waweze
kuwa ni vyombo vya ujenzi wa amani.
Baba Mtakatifu Francisko anaiomba Jumuiya
ya Kimataifa kuonesha ushirikiano wa dhati na Yordan katika kuwapokea na kuwahudumia
wakimbizi pamoja na kuendeleza harakati za ujenzi wa amani nchini Syria kwa kusitisha
vita na kuheshimu utu wa binadamu pamoja na kutoa msaada kwa wahanga wa kinzani hizi
za kijamii. Mtutu wa bunduki kamwe hauwezi kuwa ni suluhisho la matatizo ya wananchi,
kumbe kuna haja ya kuwa na mwelekeo mpya unaojikita katika majadiliano, kwa kuguswa
na mahangaiko ya watu wanaoteseka, sanjari na kutafuta suluhu ya kisiasa kwa kuwajibika
zaidi.
Mwishoni, Baba Mtakatifu amewataka vijana na walemavu kujiunga naye
kwa ajili ya kusali ili kuombea amani, kwa kutolea shida na mahangaiko yao mbele ya
Mwenyezi Mungu, kwani kwa njia hii, kweli sala zao zinakuwa na thamani kubwa. Anawataka
vijana kujibidisha katika ujenzi wa jamii inayoheshimu na kuthamini wanyonge, wagonjwa,
watoto na wazee. Hata katika shida na mahangaiko ya ndani, kamwe wasikate tamaa, watambue
kwamba, wako mbele ya Mungu na daima anawakumbuka katika sala na sadaka yake!