2014-05-24 12:53:01

Waandishi 70 wako kwenye msafara wa Papa Nchi Takatifu


Baba Mtakatifu Francisko wakati akiwa njiani kuelekea Amman nchini Yordan, amezungumza na waandishi wa habari walioko kwenye msafara wake na kuwashukuru kwa kazi kubwa wanaoifanya katika utekelezaji wa majukumu yao! Hija yake ya kitume imesheheni mambo mazito si tu kwake kama mhusika mkuu hata pia kwa waandishi wa habari ambao wanafuatilia ziara hii kwa ukaribu zaidi. Baba Mtakatifu anasema anawakumbuka katika sala zake.

Baba Mtakatifu anasema, baada ya hija yake, ana wazo la kuzungumza na waandishi wa habari watakaokuwa kwenye msafara wake. Padre Federico Lombardi msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, huu ni muujiza wa Papa Francisko kwani hata baada ya pilika pilika na ratiba ngumu kiasi hiki bado atakuwa na nafasi ya kuzungumza na waandishi wa habari wakati akirejea mjini Vatican.

Baba Mtakatifu amewashukuru waandishi wa habari 70 ambao wako kwenye msafara wake kwamba, anatambua ugumu wa hija hii, lakini ana amani na utulivu mkubwa moyoni mwake!







All the contents on this site are copyrighted ©.