2014-05-24 07:26:55

Umefunga na nani pingu za maisha?


Tupo bado kwenye chumba cha karamu ya mwisho tukisikiliza Wosia wa Yesu. Lugha inayotumika leo ni ya kimahaba, yaani, lugha ya upendo wa dhati kama ile ya wanandoa wanaopendana. Lugha hiyo ndiyo anayoitumia Yesu anapoagana na wafuasi wake, na kuwafanya kuhamasika kumsikiliza.

Katika Wosia huo ulio katika sura tano za Injili, neno upendo linatumika mara ishirini na sita. Kwa mara ya kwanza unalikuta kwenye fasuli ya leo: “Mkinipenda, mtazishika amri zangu,” au vizuri zaidi lingetumika neno: “Kama” mkinipenda. Namna hii ya kuongea kwa upande wa Yesu ni ya kinyenyekevu, ya kuaminia, ya saburi na ya kujali, yaani inajali sana uhuru na hiari ya yule anayeambiwa; kama vile angesema: “Yote yanakutegemea wewe”.

Hiyo ni lugha huru ya Yesu aliye huru. Yesu anatumia lugha ya maelewano na ya makubaliano. Kama sote tujuavyo kwamba mambo mengine yanaweza kutendeka kirahisi, kwa ari na kwa moyo wote endapo yanafanyika kwa hiari, wasemavyo waswahili: “Ukipenda utakula nyama mbichi”.

Injili ya leo ina aya saba na kwa mara saba katika kila aya Yesu anabadilisha maneno yenye wazo au mlengo moja, wa “Kuungana na mimi,” au “ kukaa ndani yangu.” Maneno hayo ni: umoja, muungano, uhusiano, nitakuwa nanyi, nitakuwa pamoja, mimi ni ndani yenu, ninyi ni ndani yangu. Katika lugha hiyo unaona kama vile Yesu anatafuta mahaba, anatafuta nafasi katika moyo wako, anataka mahusiano, tungeweza hata kusema kwamba, hapa Yesu anajigongagonga au kujipitishapitisha akiutafuta upendo wako. Kila mmoja anayo tafsiri yake juu ya neno hili upendo au mahaba.

Mtakatifu Thomas wa Aquino amefafanua neno hilo kuwa “Upendo ni hamu au hamasa ya kutaka kujiunganisha na kile unachokipenda”. Ndiyo maana Yesu hapa anahaha, anataka kujiunganisha na wewe. Anafanya hivyo kwa kutumia neno dogo sana “ndani”, anaposema: “Mimi ndani ya Baba, ninyi ndani yangu, nami ndani yenu.” Kuwa ndani, maana yake ni kuungana, kujizamisha, kuwa kitu kimoja. Kwa hiyo kupendwa kwangu na Mungu hakunitegemei mimi bali kunamtegemea Yeye. Mungu hawezi kumkatalia binadamu pendo lake hata kama huyo binadamu atalikataa pendo lake Mungu.

Anataka pia kusema kwamba, anayependa kuunganisha kwa dhati maisha yake na maisha yangu inabidi aamue kwa dhati ya moyo. Mahojiano aina hiyo hufanyika kati ya bwana na bibi arusi wakati wa kufunga ndoa. “Je unataka kuunganisha maisha yako na yangu katika mradi huu mmoja wa upendo? Ni swali kwa ajili ya kuthibitisha upendo. Ukishatoa jibu la ndiyo basi ujue hapo “umekubali sheria.” Haina maana ya kushika sheria au amri zile kumi za Musa, la hasha, bali umekubali mapendekezo yake ya upendo aliyoyaishi yeye.

Kabla Yesu alishasema “Ninawapeni amri mpya”, haikuwa na maana ya amri mbadala, bali hicho ni kitu kipya kabisa: “Pendani kama mimi nilivyowapenda, na hatimaye watu watagundua kuwa ninyi ni wanafunzi wangu.” Hiyo ni amri ya ndani ya Yesu itokanayo na maisha yake aliyoyaishi. Upendo huo ni yeye mwenyewe na maisha yake. Jinsi alivyomtii Mungu hadi akayatoa maisha yake.

Yesu anazungumzia upendo huo kwa namna ya uwingi, yaani upendo unaojizingirisha katika mazingira aina yoyote ile, upendo unaoweza kupambanua mazingira kwani unasukumwa na upendo wa Kristu, unaomwelekea jirani. Upendo ni hitaji la kutoa maisha kwa ajili ya wengine. Hivi kwa mkristu, ni kuyaiga na kuungana na jinsi hiyo ya kupenda aliyokuwa nayo Yesu. Aidha,Yesu anasema: “Mkinipenda, mtazishika amri zangu.” Na anatilia mkazo neno hili “zangu” yaani sheria zile nilizowapa mimi.

Maana yake, ukimpenda utakuwa kama yeye. Mmoja unalingana sawasawa na kile unachokipenda, unachokitamani, unachokiishi. Kushika huko maana yake ni kutunza moyoni, kuweka kama kipeo cha maisha yako. Kwa hiyo amri ya upendo inabidi iwe sehemu ya maisha yetu, iunde maisha yetu. Anayeunganisha maisha yake na yale ya Yeye, anakuwa katika hali ya kupokea zawadi itokayo kwa Baba aliyeombwa na Yesu, nayo ni Mfariji. Kama anavyosema: “Nami nitamwomba Baba naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele”.

Sifa hii ya Mfariji tunayompa Roho Mtakatifu haitoshelezi haja. Tutaelewa vizuri zaidi endapo tutatumia sifa kama vile mdhamini au mtetezi. Mtetezi huyo ni yule anayefananishwa na mtu mwenye nguvu, anayesimama kati yako na adui anayekuonea au kukupiga. Mtetezi anakukingia kifua ili usiendelee kupigika, au analinganishwa pia na yule anayekutetea mahakamani dhidi ya kesi inayokuelemea.

Mtetezi huyo anakuwa ni mtu mwenye heshima na wa kuaminika kutokana na tabia yake nzuri anasimama mahakamani badala yako. Mdhamini huyo atakutetea kwa sababu neno lake linaaminika hasa kutokana na haiba yake ya kuaminika kadamnasi. Mtu huyo ndiye anayeitwa mdhamini, mtetezi, mfariji. Yesu anaongea juu ya mdhamini au mtetezi, kwa sababu alipokuwa hapa duniani ndiye aliyekuwa anawatetea wafuasi wake dhidi ya adui. Sasa huyo Yesu hayupo tena kwa sababu anaenda kufa msalabani na hawatamwona tena kimwili. Sasa anawaahidi Roho Mfariji. Sifa za huyo Roho anazisema kuwa atakuwa “Roho wa kweli” Hiyo nguvu ya kimungu, ya mtetezi, ya mfariji, ya mdhamini atakayekuwa ndani yao daima, ni roho inayokufanya uwe wewe kweli.

Mtu halisi na wa kweli ni yule anayetenda na kuonesha kwa nje tabia ya kibinadamu iliyo ndani ya moyo wake. Jinsi unavyoongea, unavyokula, unavyotenda, unavyokunywa, unavyoburudika. Mtu anafanya hayo yote kama binadamu na siyo kama mnyama bali anafanya huku akisukumwa na upendo. Hayo ndiyo maisha ya kweli.

Kadhalika, Yesu anaposema: “Ulimwengu hauwezi kumpokea”, kadiri ya Yohane ulimwengu huo ni sehemu ile ya giza ya mamlaka, ya utawala, inayomzunguka binadamu, inayotaka kuendeleza mahusiano yale ya ubabe, ya ugandamizaji, ya chuki, ya uonezi na maisha ya ubabaishaji yasiyo ya kweli. Ulimwengu huo unawakilishwa na kila mmoja wetu. Hatuna budi kuwa macho na kuangalia kwamba ulimwengu huo unaweza kumfungia nje Yesu anayetaka tuungane naye.

Aidha Wosia unasema: “Roho huyo mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu”. Huyo roho ni yule aliyewaosha miguu wanafunzi wake, aliyeonesha upendo kwa Yuda aliyekuwa mbioni kwenda kumsaliti. Roho hiyo ya upendo iliyo katika Yesu itakuwa ndani ya wafuasi wake. Baada ya muda mfupi Yesu atakapokuwa Msalabani atawapa huyo Roho kwa wanandoa wake.

Mahusiano au muunganiko huo na Yesu utadumu milele, ndiyo maana anasema: “Sitawaacha ninyi yatima”, nitaendelea kuwa nanyi. Katika mipaka ya ulimwengu huu utokanao na umbali, homa na vifo, uwepo wa Yesu ndani mwangu ni chemchemi inayodumu. Huwezi kamwe kuachwa yatima.

“Bado kitambo kidogo na ulimwengu haunioni tena”. Huo ni ulimwengu unaomwona Yesu kibaolojia, ambao ulimwona Yesu mara moja na baadaye ameisha vibaya msalabani. Huo ndiyo mtazamo wa ulimwengu. Lakini wafuasi wake wanamwona Yesu kwa macho ya kiroho. Mungu ndiye atakayewafanya wamwone Roho huyo. “Siku ile ninyi mtatambua ya kuwa mimi ni ndani ya Baba yangu, nanyi ndani yangu, nami ndani yenu.”

Umoja huo wa maisha, wenye alama ya upendo, kama zawadi toka kwa Baba wa mbinguni unatuunganisha katika fumbo hili la Utatu. Hatima ya fasuli hii ndiyo “Naye anipendaye atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda na kujidhihirisha kwake.” Ni mwito wa kupokea maneno haya ya mwisho ya Yesu, ni mwanzo pia wa kuchagua maisha kama tunataka kuwa na maisha ya kweli.

Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.