Papa Francisko aanza hija yake ya kichungaji Nchi Takatifu
Baba Mtakatifu Francisko ameondoka mjini Roma asubuhi, tarehe 24 Mei 2014 tayari kwa
hija ya kitume huko Yordani, Palestina na Israeli kama kilele cha maadhimisho ya Jubilee
ya Miaka 50 tangu Papa Paulo VI alipokutana, akazungumza na kusali pamoja na Patriaki
Anathegoras wa Yerusalemu, huu ukawa ni mwanzo mpya wa mchakato wa majadiliano ya
kiekumene.
Baba Mtakatifu katika Uwanja wa ndege wa Fiumicino, Roma amesindikizwa
na viongozi mbali mbali wa Kanisa na Serikali ya Italia. Ametumia nafasi hii kuwasalimia
mmoja mmoja na kuwatakia kheri na baraka. Kama desturi, Baba Mtakatifu alibeba mkoba
wake mweusi tayari kuanza safari ya kitume Nchi Takatifu.
Baba Mtakatifu amewaandikia
wakuu wa Nchi ya Italia, Ugiriki, Cyprus na Israeli ujumbe wa matashi mema wakati
alipokuwa anasafiri kuelekea mjini Amman, kituo cha kwanza cha hija yake ya kitume!
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliomwandikia Rais Giorgio Napolitano wa Italia,
anamwambia kwamba, anaelekea Nchi Takatifu ili kuadhimisha Jubilee ya Miaka 50 tangu
Papa Paulo VI alipokutana na Patriaki Anathegoras wa Yerusalem pamoja na kusali kwa
ajili ya kuombea haki, amani pamoja na kukoleza majadiliano ya kiekumene na kidini.
Anawatakia kheri na baraka wananchi wa Italia, anawaomba pia kumkumbuka katika sala
zao.
Naye Rais Giorgio Napolitano wa Italia amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko
na kwamba, Jumuiya ya Kimataifa ina matumaini makubwa katika hija hii ya kitume huko
Nchi Takatifu, mahali ambapo kuna kinzani kubwa katika historia yake na ulimwengu
kwa ujumla. Ni matumaini ya Rais Napolitano kwamba, hija hii itakuwa ni cheche za
matumaini kwa wale wanaotaka kusimama kidete kuendeleza amani na utulivu. Rais Napolitano
anamtakia mafanikio mema katika hija hii ya kitume.
Baba Mtakatifu Francisko
katika ujumbe wake kwa Rais Karolos Paoulias wa Ugiriki anamtakia mafanikio mema katika
kukuza na kudumisha misingi ya haki na amani, anawaombea baraka tele kutoka kwa Mwenyezi
Mungu.
Baba Mtakatifu Francisko akimwandikia Rais Nicos Anastasides wa Ugriki
anasema, anawatakia kheri na baraka tele wananchi wa Ugiriki na kwamba, anawaombea
furaha na amani kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko
amemwandikia pia ujumbe Rais Shimon Peres wa Israel kwa kumtakia matashi mema na wananchi
wote wa Israeli na kwamba, ana matumaini ya kukutana naye Nchi Takatifu wakati wa
hija yake ya kichungaji. Anawatakia wote baraka tele!