2014-05-24 12:55:28

Padre Mario Vergara na Katekista Isidore Ngei Ko Lat watangazwa kuwa wenyeheri!


Kardinali Angelo Amato, Rais wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu, katika maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria msaada wa Wakristo inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 24 Mei, amewatangaza Watumishi wa Mungu Padre Mario Vergara, Mwanashirika kutoka Taasisi ya Kipapa ya utume wa nje, PIME, Italia na Katekista Isidore Ngei Ko Lat kutoka Burma kuwa Wenyeheri. Wenyeheri hawa wapya waliuwawa kikatili kutokana na chuki za kiimani kunako mwaka 1950 nchini Burma.

Ni matumaini ya Mama Kanisa kwamba, ujasiri na ushujaa wa imani ulioneshwa na Wenyeheri hawa wapya, utakoleza ari na moyo wa kimissionari hususan miongoni mwa Makatekista, wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa hasa katika Nchi za Kimissionari. Kanisa linawashukuru kwa sadaka na majitoleo yao.

Mwenyeheri Padre Mario Vergara alizaliwa mjini Frattamaggiore kunako mwaka 1910. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapewa Daraja takatifu la Upadre tarehe 28 Agosti 1934. Alitekeleza maisha na utume wake wa Kipadre katika mazingira magumu na hatarishi, akasaidiwa na Makatekista. Wakati wa Vita kuu ya Pili ya Dunia kunako Mwaka 1941, akakamatwa na kufungwa kwenye kambi ya Waingereza nchini India, ambako alitumikia kifungo kwa muda wa miaka 4.

Alipoachiliwa huru alirudi nchini Italia na baadaye akakata shauri ya kurudi nchini Burma kuendelea na utume wake, akaona Burma ikijipatia uhuru wake kutoka kwa Mwingereza kunako mwaka 1948. Lakini baada ya muda mfupi Burma ilijikuta inatumbukia katika machafuko ya kisiasa na kijamii, Padre Mario Vergara, akajitokeza kuwa ni sauti ya wanyonge, kiasi cha kuchukiwa na waasi wa Serikali ya Burma.

Tarehe 24 Mei 1950 wakati Padre Vergara na Katekista Isidore Ngei Ko Lat walipokwenda kuomba kuachiliwa kwa Katekista mmoja aliyekuwa amekamatwa na kufungwa gerezani walikutana na kiongozi wa waasi, baada ya kuwahoji sana, akaamuru watiwe pingu na hatimaye kuuwawa kikatili. Miili yao iliyofungwa kwenye mfuko na kutupwa mtoni.

Katekista Isidore Ngei Ko Lat, anakuwa ni mwamini wa kwanza kabisa katika historia ya Kanisa Katoliki nchini Burma kutangazwa kuwa Mwenyeheri. Yeye alibatizwa tarehe 7 Septemba 1918. Ni kijana aliyekulia katika mazingira ya Kanisa, akawasaidia Wamissionari katika utume wao. Akajiunga na Seminari ndogo huko Toungoo, akaonesha ari na moyo wa kutaka kuwa Padre, lakini afya yake ilikuwa mbaya, kiasi cha kumfanya kushindwa kuendelea na masomo. Lakini aliendelea kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake kama mwamini mlei, bila kuoa, akafunga shule binafsi, mahali ambapo alifundisha Katekesi.

Kunako mwaka 1948 akakutana na Padre Vergara aliyemwalika kufundisha Katekesi mjini Shadaw. Mama Kanisa anawashukuru kwa majitoleo yao, leo hii wameandikwa kwenye orodha ya Wenyeheri ndani ya Kanisa.








All the contents on this site are copyrighted ©.