Kuna watu wenye mapenzi mema wanaotaka kuona amani ikitawala duniani!
Mfalme Abdalla wa Pili wa Yordan amemkaribisha Baba Mtakatifu Francisko nchini mwake
kwa kumwambia kwamba, dunia inakabiliana na changamoto mbali mbali zinazotokana na
watu kutoaminiana na kutokubali mabadiliko wala kuheshimiana. Yordan ni nchi ya watu
wenye imani thabiti. Anasema kuna haja ya kuunganisha sauti za watu wote wenye mapenzi
mema, ili kuheshimiana, kujenga na kudumisha amani pamoja na uchaji wa Mungu bila
kusahau majadiliano ya kidini.
Mfalme Abdalla anasema duniani bado kuna watu
wenye mapenzi mema wanaopenda kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya
binadamu; amani na utulivu. Anamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa
kuwa ni mfano bora wa kuigwa katika kutetea haki msingi za binadamu pamoja na kuendeleza
majadiliano ya kidini, ili kujenga daraja la amani, kama ilivyo pia kwa Yordan.
Anasema,
nchi yake inaendelea kuhimiza umuhimu wa kujenga jamii inayosimikwa katika msingi
wa amani na utulivu, huruma na haki kwa kuwakata watu wanaotaka kujenga chuki na uhasama
kati ya watu, bali kudumisha amri ya upendo kwa Mungu na jirani. Anapenda kuiona dini
ya Kiislam ikijisimika katika amani na utulivu. Anampongeza Papa Francisko kwa kutembelea
Mto Yordan mahali alipobatizwa Yesu. Yordan itaendelea kushirikiana na watu wote wenye
mapenzi mema katika ujenzi wa misingi ya haki, amani na utulivu, ili kukabiliana na
changamoto zinazojitokeza katika maisha ya mwanadamu.