Patriaki Bartolomeo wa kwanza anasema, Mwaka 1964 umeacha alama ya kudumu katika historia
na maisha ya Kanisa katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Hapa Wakristo wamejifunza
kusameheana kutokana na makosa ya kihistoria na hivyo kuanza kujifunga kibwebwe kwa
ajili ya ujenzi wa misingi ya upatanisho wa kweli!
Papa Francisko anaendeleza
mchakato huu kwa imani na matumaini makubwa tangu alipoanza utume wake kama Khalifa
wa Mtakatifu Petro, katika mwangwi wa maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 tangu Papa
Paulo VI alipokutana na kusali pamoja na Patriaki Anathegoras wa Yerusalemu. Hili
lilikuwa ni tukio la majadiliano ya kiekumene yanayojikita katika upendo na ukweli,
nguzo kuu na dira katika majadiliano ya kiekumene!
Kanisa Katoliki na Kanisa
la Kiorthodox kwa sasa wameanza ukurasa mpya kabisa baada ya Makanisa haya mawili
kutembea katika giza la chuki na uhasama wa kihistoria na kuweka pembeni mambo msingi
yanayowaunganisha kama Wakristo, yaani: Biblia Takatifu na Mapokeo ya Kanisa.
Makanisa
haya yalikuwa yameingiwa na kishawishi cha kujisikia kuwa yanaweza kujitosheleza na
kujitegemea pasi ya kuhitaji uwepo na ushirikiano wa Makanisa mengine! Tarehe 5 Januari
1964 ukawa ni mwanzo mpya wa hija ya majadiliano ya kiekumene kati ya Makanisa kwa
kujikita katika mchakato wa upatanisho na majadiliano ya upendo katika ukweli, kiasi
cha kuanza kuimarisha ari na moyo wa upendo na heshima kati ya Wakristo! Ya kale yamepita,
sasa tugange yaliyopo na yale yajayo anasema Patriaki Bartolomeo wa kwanza.
Tume
ya pamoja na majadiliano kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox katika kipindi
cha miaka 50 imechapisha nyaraka mbali mbali zinazoyasaidia Makanisa haya mawili kujadiliana
pamoja na kukumbuka kwamba, wanapaswa kutekeleza agizo la Kristo, yaani wote wawe
wamoja, kauli mbiu inayoongoza hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko katika
Nchi Takatifu. Wakristo hawana njia mbadala bali kuendeleza mchakato wa upatanisho
na umoja wa Kanisa kama sehemu ya utekelezaji wa mapenzi ya Kristo kwa wafuasi wake!
Patriaki
Bartolomeo wa kwanza anasema, hivi karibuni aliitisha Mtaguso mkuu uliowashirikisha
wakuu wa Makanisa ya Kiorthodox yaliyoenea sehemu mbali mbali duniani na kuamua kwamba,
kunako Mwaka 2016 uadhimishwe Mtaguso mkuu wa Makanisa ya Kiorthodox Duniani, kielelezo
cha umoja na mshikamano kati ya Makanisa ya Kiorthodox ili kuweza kukabiliana na changamoto
zinazojitokeza katika ulimwengu mamboleo.
Papa Francisko amekwisha julishwa
kuhusu maadhimisho haya na kuunga mkono juhudi hizi ili kuendeleza majadiliano ya
kiekumene kati ya Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiorthodox. Mkutano kati ya Papa Francisko
na Patriaki Bartolomeo wa kwanza, Jumapili jioni mjini Yerusalem utakuwa ni kielelezo
cha utashi wa Makanisa kuendeleza hija ya majadiliano ya kiekumene yanayojikita katika
upendo na uaminifu kwa kweli za Kiinjili, mchakato ambao umeanzishwa miaka 50 iliyopita.
Umefika wakati wa kushikamana na kushuhudia Ukristo hata katika madhulumu na pale
ambapo haki, amani na upendo vinakosekana. Umefika wakati wa kusimama kidete kwa pamoja
kulinda na kutetea kazi ya uumbaji anasema Patriki Bartolomeo wa kwanza.
Upatanisho
ni changamoto kubwa kwa sasa kuliko hata ilivyokuwa miaka 50 iliyopita na kwamba,
Mkutano wake na Papa Francisko ni tukio kubwa la kihistoria, ili kwa pamoja kusonga
mbele kwa imani na matumaini ili kukuza na kudumisha msingi wa majadiliano, amani
na utulivu, tayari kufuata nyayo za watangulizi wao katika huduma kwa Kristo na Kanisa
lake.
Hii ni nafasi ya kuwaalika watu wote wenye mapenzi mema kujikita katika
majadiliano ya kweli za Kiinjili na furaha ya kukutana na Yesu Kristo Mfufuka. Jambo
hili linawezekana pale tu Makanisa yatakapofaulu kuganga migawanyiko na tofauti zake
za ndani, ili upendo na furaha viweze kukamilika katika maisha ya Wakristo!
Miaka
50 imewafunda wakristo kusameheana na kujipatanisha wao kwa wao, ili umoja na mshikamano
viweze kutawala tena kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo na Kanisa lake. Tarehe
25 Mei 2014 ni tarehe itakayokumbukwa katika maisha na utume wa Kanisa!