Hotuba ya Papa kwa viongozi wa Serikali ya Yordan!
Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kuwasili mjini Amman, Jumamosi mchana 24 Mei
2014 alimtembelea Mfalme Abdallah wa pili pamoja na familia yake baadaye amekutana
na kuzungumza na viongozi wa Serikali kwenye Ikulu ya Mfalme. Baba Mtakatifu amemshukuru
Mwenyezi Mungu kwa kumpatia fursa ya kutembelea Yordan akifuata nyayo za watangulizi
wake Papa Paulo VI, Yohane Paulo II na Benedikto XVI.
Anakumbuka mkutano wao
wa pamoja uliofanyika mjini Vatican hivi karibuni. Anasema, Yordan ni nchi ambayo
ina utajiri mkubwa wa kidini kutokana na uwepo wa dini ya: Kiyahudu, Kikristo na Kiislam.
Ni nchi ambayo imeonesha ukarimu mkubwa kwa wakimbizi kutoka Palestina, Iraq na maeneo
ambayo bado kuna vita na kinzani za kijamii kama vile Syria. Ukarimu huu unapaswa
kuheshimiwa na kuungwa mkono na Jumuiya ya Kimataifa. Kanisa Katoliki kadiri ya uwezo
wake, linapenda kuendelea kutoa huduma kwa wakimbizi na wahitaji kwa kutumia Shirika
la Misaada la Caritas, Yordan.
Baba Mtakatifu anasikitishwa na vita pamoja
na kinzani zinazoendelea huko Mashariki ya Kati, anapenda kuchukua fursa hii kuwashukuru
viongozi wa Yordani kwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kutafuta amani ya
kudumu katika Ukanda huu na kwamba, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, suluhu ya kudumu
inapatikana nchini Syria sanjari na mgogoro kati ya Israeli na Palestina.
Baba
Mtakatifu anaishukuru Jumuiya ya Waislam chini ya uongozi wa Mfalme Abdalla II kwa
kuendeleza tunu msingi za mafundisho ya dini ya Kiislam zinazojikita katika amani
na utulivu kati ya waamini wa dini mbali mbali. Anaipongeza Serikali kwa kuanzisha
majadiliano ya kidini na uelewano mwema kati ya Wayahudi, Waislam na Wakristo sanjari
na kushiriki katika juma la utulivu kati ya dini, ililoanzishwa na Umoja wa Mataifa.
Baba
Mtakatifu anaishukuru na kuipongeza Jumuiya ya Kikristo ambayo imeendelea kushiriki
katika kuchangia mafao ya wengi ndani ya Jamii na hata katika uchache wao, wamekuwa
na mchango mkubwa katika sekta ya elimu na afya, huduma ambazo zinatolewa bila ubaguzi
na watu wanaendelea kuungama imani yao katika hali ya utulivu, huku wakiheshimu uhuru
wa kidini, msingi wa haki zote za binadamu.
Ni matumaini ya Baba Mtakatifu
kwamba, haki hii itaheshimiwa katika Ukanda wa Mashariki ya Kati kwa mtu binafsi au
kundi la watu. Wakristo wanajisikia kuwa ni sehemu ya raia wa Nchi zao na wanataka
kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ujenzi wa jamii kwa kushirikiana na waamini
wa dini ya Kiislam, kwa kutoa mchango wao wa dhati.
Baba Mtakatifu anawatakia
wananchi wa Yordan amani na maendeleo na kwamba, hija hii ya kitume isaidie mchakato
wa kutafuta na kuendeleza mahusiano mema kati ya Wakristo na Waislam. Mwishoni, Baba
Mtakatifu amemtakia Mfalme Abdallah wa Pili maisha marefu na baraka tele!