Baba Mtakatifu Francisko anaianza hija yake ya kitume kwa kutembea Amman nchini Yordan.
Hapa kuna mambo makuu matatu ya kukumbuka: hapa kuna changamoto ya kimissionari, kinabii
na chemchemi ya maisha ya Kikristo.
Padre Samir Khalid Samir anasema, Yordan
ni mahali ambapo watu kutoka katika tamaduni, lugha na jamaa wanakutana, kumbe, ni
sehemu muhimu sana katika kudumisha utamaduni na misingi ya maisha ya Kiristo huko
Mashariki ya Kati, hali ambayo wakati mwingine inasababisha kinzani na migongano ya
kijamii. Ni jukumu la Wakristo na Waamini wa dini mbali mbali kudumisha majadiliano
ya kiekumene na kidini, ili haki, amani na utulivu viweze kutawala!
Majiundo
makini: kiroho, kimwili na kiakili yatawasaidia waamini kuweza kufahamiana, kupendana
na kushikamana kama ndugu, ili kuondokana na falsafa na kinzani zilizojitokeza katika
historia ya watu wanaoishi huko Nchi Takatifu, ndiyo maana Kanisa limewekeza kwa kiasi
kikubwa katika Chuo Kikuu cha Madaba, ili vijana wajifunze utamaduni wa kuheshimiana
na kuthaminiana, kwani wao ndio tegemeo la jamii katika ujenzi wa misingi ya haki,
amani na utu na umoja, kama alivyosema Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI wakati
anaweka jiwe la msingi katika ujenzi wa Chuo Kikuu cha Madaba.
Utu na heshima
ya binadamu ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, kwa kukazia pia uhuru
wa kidini.
Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko inapania pamoja na mambo
mengine kuimarisha ari na mwamko wa kimissionari miongoni mwa Wakristo wanaoishi Nchi
Takatifu, kwani wao ni mashahidi wa mambo yale ambayo waliyasikia, wakayaona na kuyashuhudia
katika maisha, kwani Fumbo la Pasaka ni kiini cha imani na matumaini ya Watu wa Mungu.
Kwa kifo na ufufuko wake, Yesu amemkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi
na mauti.