Papa Francisko ni mjumbe wa majadiliano ya kiekumene, kidini na amani
Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Nchi Takatifu imesheheni matukio muhimu
sana katika maisha na utume wa Kanisa katika mchakato wa kukuza na kudumisha majadiliano
ya kiekumene na kidini sanjari na kukoleza maendeleo ya binadamu yanayosimikwa katika
misingi ya haki, amani na mshikamano wa kidugu. Hii ni hija ambayo ni mwendelezo wa
historia ya Mapapa inayowaunganisha na Nchi Takatifu, chimbuko la Kanisa la Kristo.
Papa
Paulo VI aliwashangaza sana Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican alipoamua kutembelea
Nchi Takatifu, ili kukutana, kuzungumza na kusali pamoja na Patriaki Anathegoras wa
Yerusalemu, kama mwanzo mpya wa mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Hii ilikuwa
ni mara ya kwanza kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro kutembelea rasmi Yerusalemu pengine
na kuwashangaza walimwengu kwa kupanda ndege kwa mara ya kwanza, mwelekeo mpya katika
maisha na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Baada ya miaka thelathini na
sita, Mtakatifu Yohane Paulo II alitembelea tena Nchi Takatifu katika maadhimisho
ya Jubilee kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI akatembelea
tena huko mwaka 2009. Kumbe, hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko inaendeleza
mchakato wa majadiliano ya kiekumene ulioanzishwa na watangulizi wake, miaka hamsini
iliyopita; majadiliano yanayowakutanisha Watakati Petro na Andrea kwa ajili ya ustawi
na maendeleo ya Kanisa la Kristo.
Ni mkutano kati ya ndugu wawili katika Kristo
kwani viongozi mbali mbali wa Makanisa ya Kikristo walioko katika Nchi Takatifu wanatarajiwa
kushiriki katika tukio hili la kihistoria, ili kusali kwa pamoja kuzunguka Kaburi
la Yesu Kristo Mfufuka, ili wote wawe wamoja! Ni hija inayojikita pia katika kukoleza
majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na waamini wa dini mbali mbali wanaoishi katika
Nchi Takatifu, ili kwa pamoja waweze kujifunga kibwebwe kutafuta na kudumisha amani,
upendo na mshikamano wa kidugu, kwa kutambua kwamba, wote wanaunda Familia moja ya
binadamu!
Taarifa kutoka Nchi Takatifu zinaonesha kwamba, waamini na watu wote
wenye mapenzi mema wako tayari kumpokea Baba Mtakatifu Francisko anapowatembelea kuanzia
Jumamosi tarehe 24 hadi Jumatatu tarehe 26 Mei 2014. Sehemu nyingi zinakamilisha maandalizi
ya mwisho mwisho kabla ya Baba Mtakatifu Francisko "ajatinga timu" huko Mashariki
ya Kati!