Katika dini nyingi iko desturi nzuri ya kiroho ya kufanya hija pahala patakatifu au
sehemu za kihistoria za dini hiyo. Hija hiyo mara nyingi hufanyika kama moja ya kuadhimisha
tukio fulani muhimu linalomhusu mtu binafsi ili kujichumia neema anayohitaji mhiji
au alhaji.
Papa pia hufanya
hija sehemu mbalimbali kama vile Lourdes, Fatima, Loreto, Namugongo, Nchi Takatifu,
nakadhalika. Hija ya Papa haiwi kwa ajili yake binafsi tu, bali hasa ni kuchuma neema
kwa ajili ya kanisa zima, pia inakuwa kwa ajili ya kuimarisha mahusiano ya kuletesha
haki, amani na upendo kati ya nchi na nchi.
Mwaka huu kuna jubilei za dhahabu
kadhaa za kikanisa zitokanazo na Mtaguso wa pili wa Vatican. Zaidi pia ni mwaka wa
50 tangu Papa Paulo VI alipohiji nchi ya ahadi na kuzungumza na Patriaki Anathagora
wa Yerusalemu. Papa Fransis atahiji nchi ya ahadi ikiwa ni kuadhimisha jubilei ya
dhahabu ya hija hiyo ya Papa Paulo VI. Katika hija hiyo, Papa atakutana na viongozi
muhimu wa serikali na dini, atakutana pia na waumini wenzetu walioko huko.
Papa
atazuru sehemu chache muhimu. Mosi, ataenda Bethlehemu kuzuru na kusali pahala alipozaliwa
Yesu. Ataenda kuzuru na kusali kando ya mto Yordani alikobatizwa Yesu. Mwisho ataenda
kuangalia chumba ambacho Yesu alikula Karamu ya Mwisho na mitume wake. Chumba hicho
ni mandhali ya mwisho aliyokuwa Yesu kabla ya kuteswa na kufa kwake.
Kwa hiyo
wakristu wote tunaalikwa mosi, kuiombea hija hii ya Papa, kusudi asafiri salama, aende
akatuombee na kufanikisha makusudio aliyojipangia kwa faida yake, na kwa manufaa ya
kanisa zima na ulimwengu kijumla, na hatimaye arudi salama, kusudi Mungu atukuzwe
katika yote. Pili tunaalikwa sisi sote kutanguzana na Papa kwenda katika hija hiyo,
usikose kuwepo katika msafara huo wa Baba Mtakatifu. Kutokana na msongamano wa watu
na hasa kupanda gharama ya maisha, siyo wote watafanikiwa kwenda hiyo hija.
Tunaalikwa
kukata tiketi ya kiroho ambayo gharama yake ni bure sanasana inategemea uhuru wako
mwenyewe, na mkatishaji tiketi ni Roho Mtakatifu mwenyewe ambaye hata Yeye mwenyewe
ataenda kwenye hija hiyo ya awali tangu atoke huko alipokufa Yesu Msalabani. “Akainama
kichwa akaitoa Roho yake”.
Kwa watakaoenda huko kwa tiketi ya Roho Mtakatifu,
mnaalikwa kusoma ramani hii au mwongozo ufuatao, utakaowasaidia kujua sehemu mbalimbali
mtakazotembelea na kuzihiji pindi mnaongozana na Papa. Hizo ni sehemu muhimu ambazo
kulifanyika mambo makuu na mazito yahusuyo ukombozi wetu.
Katika mwongozo
huu tutajaribu kuzieleza kwa kifupi sana sehemu hizo kijiografia na kiteolojia. Tutaona
pia matukio yaliyotokea sehemu hizo, yahusuhuyo Yesu au mitume wake na sisi tunaweza
kupata fundisho gani toka sehemu hiyo. Hebu twendeni kwanza Betlehemu alikozaliwa
Yesu tuhimizane kwenda huko kwa maneno ya Wachungaji waliokuwa wanahimizana kwenda
huko baada ya kupata taarifa toka kwa malaika: “Twendeni mpaka Betlehemu, tukashuhudie
tukio hilo alilotujulisha Bwana.” (Lk 2:15).
“TWENDENI MPAKA BETLEHEMU” Lk
2:15
Jina hili Bethlehemu linatokana na maneno mawili ya Kiebrania, Bet ni
nyumba na Lehem (lexem) ni mkate, kwa hiyo Beth-Lehem au bet-lexem maana yake nyumba
ya mkate. Kwa lugha ya kigiriki cha zamani walitamka Bethleem. Ziko sehemu nyingi
zenye nyumba ya mkate mathalani Beth-lehem-ephratah, Bethlehemjudah, lakini Bethlehemu
iliyokuwa kusini karibu na Yerusalemu ndiyo iliyokuwa inaitwa Bethlehemu katika mji
wa Daudi. Hapo ndipo alipozaliwa Yesu. Ni mji ambao toka zamani wameishi wakristu
wengi, lakini sasa wanaishi pia watu wa dini mchanganyiko. Sehemu hii wanafurika wahaji
na watalii wengi sana hususani wakati wa Kipindi cha Noeli.
Kisa cha kujulikana
Betlehemu kilianza na safari ya Yosefu na Maria aliyekuwa na baraka tumboni. Walienda
huko kwa ajili ya senza. Katika pilikapilika za kutafuta mahali pa kulala mama akajifungua
mtoto wake hapo Betlehemu mji wa Daudi (Lk. 2:4). Baada ya kuzaliwa, mtoto huyo akaviringishwa
nguo za mtoto mchanga na kulazwa kwenye hori la kulishilia wanyama. Hii ndiyo alama
ambayo malaika waliwapa maelezo wachungaji na kuwaagiza waende huko kumwona mtoto.
Malaika wakawaambia wachungaji: “Leo katika mji wa Daudi amezaliwa kwa ajili yenu,
Mwokozi, ndiye Kristu Bwana. Na hii ndiyo ishara kwenu; mtamkuta mtoto mchanga amevikwa
nguo za kitoto, amelala katika hoi ya kulia ng’ombe.”
Kumbe yawezekana malaika
walikuwa wa kwanza kufika hapo Betlehemu na kushuhudia mambo yalivyo kabla ya kwenda
kuwahabarisha wachungaji. Tunaambiwa pia kwamba mara tu baada ya malaika kuondoka,
wachungaji nao wakaambizana wenyewe, Jamani tusiilazie damu taarifa hii ya malaika:
“Twendeni mpaka Betlehemu, tukashuhudie tukio hilo alilotujulisha Bwana.” (Lk. 2:15).
Baada ya kumwona mtoto wakaanza nao wakaanza kutawanya habari: “Walipomwona (mtoto
Yesu) wakatoa habari waliyoambiwa juu ya huyo mtoto. Halafu wote waliosikia wakastaajabu
kwa hayo waliyoambiwa na wachungaji.” (Lk 2:27).
Malaika walipoona utukufu
umetua Bethlehemu, hawakuuacha utulie tu pale pangoni, bali wakaondoka kwenda kuutangaza
kwa wachungaji. Kwa hiyo utukufu haukuhusu pango ila unawahusu wachungaji wanaowakilisha
wanyonge wote. Wachungaji ndiyo wanaodhihirisha utukufu wa Mungu. Mungu anajidhihirisha
na kutukuzwa pale tu ambapo wanyonge, fukara wanapofurahi. Huo ni utukufu wa Mungu.
Wachungaji
wanafurahi kwa sababu kutokana na hali halisi ya unyonge wao, walijisikia kama watu
waliolaaniwa, kwa hiyo hawakutegemea kabisa kupata mawasiliano na Mungu.
Kumbe,
amezaliwa mchungaji mwenzao, anayejua unyonge wao. Hawakujiamini wenyewe, na mara
moja wakaanza kushauriana wenyewe na kuchukua maamuzi ya kwenda kushuhudia na baadaye
kutoa ushuhuda. “Twendeni mpaka Betlehemu, tukashuhudie tukio hilo alilotujulisha
Bwana.” Wanaenda haraka, kushuhudia utukufu wa Mungu, ambao ni kutaka watu wapate
furaha haraka.
Kwetu sisi tungetegemea kusikia mambo ya ajabu zaidi au hata
kusikia muujiza. Hakuna maelekezo zaidi, ni kama vile amezaliwa mtoto wa kawaida.
Maisha ya kawaida yanaendelea. Yesu kuwa Mungu hakutegemei muujiza wa pekee, bali
yeye mwenyewe jinsi alivyo. Yeye ni kama sisi, Mungu amekuwa mwenzetu. Anayemtegemea
Mungu wa kufanya miujiza, ujue mungu aina hiyo ni mungu wa kipagani.
Wachungaji
wanaenda Betlehemu na wanamwona mtoto aliyeviringishwa nguo. Hiyo ndiyo picha mpya
ya Mungu anayejidhihirisha kwa binadamu. Watoto waliviringishwa nguo ili kuwakinga
na baridi lakini pia inayo maana ya kidini. Mtoto ni safi, hivi huwezi kumshika tu
kwa mikono, lakini kuna maana pia muhimu ya kiroho, hasa mwinjili anaposisitiza jinsi
mtoto alivyoviringishwa nguo, hoja kubwa ni kusudi mtoto huyo aweze kuguswa, kushikwashikwa
na kubebwa na watu wote.
Aidha imeandikwa mara tatu kuwa aliwekwa katika hori
la kulishia chakula wanyama (ng’ombe). Kwa hiyo msisitizo huo unahusu chakula. Mtoto
aliviringishwa nguo, kama vile mkate unavyoviringishwa karatasi au majani na kuwekwa
kwenye nyumba ya mkate (Bethlehemu). Kwamba Yesu anadhihirishwa hapa kama mkate yaani
chakula. Malaika wanawaelekeza wachungaji kwenda kwenye nyumba ya mkate (bethlehemu)
huko watauona mkate umeviringishwa.
“Na hii ndiyo ishara kwenu; mtamkuta mtoto
mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelala katika hoi ya kulia ng’ombe.”Yesu aliishi
na kuhitimisha historia ya maisha yake hapa duniani akijionesha mwenyewe daima kuwa
ni mkate utokao mbinguni. Maisha yake yote akayatolea hadi chembe ya mwisho ya mkate.
“Twendeni mpaka Betlehemu, tukashuhudie tukio hilo alilotujulisha Bwana.”
Wachungaji
wanapofika pangoni wakamwona Maria, Yosefu na mtoto mchanga amelala horini. Hawaoni
cha pekee zaidi. Kisha wakatoa taarifa juu ya kile walichoambiwa juu ya huyo mtoto.
“Walipomwona (mtoto Yesu) wakatoa habari waliyoambiwa juu ya huyo mtoto. Halafu wote
waliosikia wakastaajabu kwa hayo waliyoambiwa na wachungaji.” Nadhani watu wote walishangazwa
na taarifa hizo kwani ni Mungu aina gani anayeweza kuwatokea watu wanyonge kama wachungaji.
Kama ndivyo basi hayo ni maajabu.
Tunaambiwa jambo jingine lililotokea pale
Bethlehemu ni kuwa Maria akayaweka maneno hayo yote, akiyafikiri moyoni mwake. Neno
kufikiri, siyo tafsiri sahihi, kwa kigiriki “sinmbalus” inamanisha kuweka mambo pamoja
na kutafakari, hasa kule ambako mmoja unapoona mambo lakini unashindwa kuyaelewa.
Maria anatulia, anaangalia, anaunganisha mambo anaweka pamoja mambo yanayomtukia.
Atakuja kufahamu atakapokuwa amesimama chini ya Msalaba.
Wachungaji wanaondoka
wakimshukuru na kumsifu Mungu – wameyaona maisha mapya. Wamemwona Mungu aliyejifanya
binadamu na kulingana na watu. Wamemwona Mungu anayejiacha kushikwashikwa na watu
wenye mikono michafu, watu wanaonuka, yaani wanyonge, maskini, wazee, wenye dhambi,
walalahoi. Watu hawa wanyonge wameona na wanafurahi, wanamshukuru na kumsifu Mungu,
kisha wanamshuhudia. Kumbe watu hawa wanyonge tu ndiyo wanaoweza kutambua na kushabikia
sera hii kubwa ya Mungu kujifanya mtu. Ni watu kama hawa ndiyo wanaoweza kuwa na furaha,
na kusifu na kumshukuru Mungu. Kwa wataalamu, wakuu, matajiri sera hii haiingii akili
na mioyoni mwao.
Ni muhimu hata kwetu kwamba badala ya kujihoji na kufikri
nini tufanye nini katika maisha, baada ya kumwona Kristu tubaki tu kufurahi. Tumeona
tendo kuu la upendo alilotufanyia Mungu. Huo ndiyo mwanzo wa uchumba kati ya Mungu
na binadamu, kati ya Yesu na Kanisa lake. Sisi tunafunganishwa na Yesu katika upendo.
Ndiyo mwanzo wa maisha ya upendo na ya furaha. Wanaopendana daima wanashika simu mkononi
wakisubiri ”message au kupib”, au kuitwa na mpendwa wao ili kuongeana.
Sisi
tukitaka kugundua utukufu na upendo huo wa Mungu tuanza Bethlehemu, na kuendelea mbele
hadi kwenye majitoleo kamili ya Yesu kule Kalvari. Kwa hiyo ndugu zangu “twendeni
na Papa mpaka Betlehemu” tukirudi toka huko tuwapagawaze watu kwa tutakayoyaona. Hebu
sasa tutoke Bethlehemu kuongozane na Papa hadi mto Yordani.
“YESU ALIRUDI
KUTOKA GALILAYA MPAKA YORDANI KWA YOHANE ILI ABATIZWE” Mt 3: 13
Baada ya
kuzaliwa, kukimbilia Misri na kurudi toka huko, Yesu akaenda na wazazi wake kukaa
Galilaya (nyumbani kwake) kwa miaka hii 33. Kabla ya kuanza utume rasmi Yesu anaenda
Yordani kubatizwa na Yohane. Baada ya kubatizwa anaenda Kafarnaum na huko ndiko anaanza
kazi ya kuhubiri. Ebu tuangalie pahali hapa alipobatizwa Yesu. Kwa kawaida, Yohane
mbatizaji alikuwa upande wa mashariki, ng’ambo ya mto Yordani (Galilaya ya Upagani).
Huko akawabatiza watu na kuwataka wauvuke tena mto Yordani na kuingia Magharibi yaani
nchi ya ahadi. Akawasadikisha watu kwamba sehemu hiyo ya ubatizo ilikuwa ni sehemu
halisi ambayo Musa angewaingiza watu katika nchi ya ahadi, walipofika toka utumwani
Misri. Kwa hiyo, wale wote waliojidhani kwamba wameingia nchi ya ahadi kumbe walikuwa
bado hawajakuingia kidhati.
Kwa hiyo, Yohane akawaita watu toka Yudea warudi
tena ng’ambo ya Yordani ili wabatizwe upya, na kuingia nchi ya ahadi kama ilivyokuwa
walipotoka Misri. Watu wakafika pahala hapo palipokuwa opanaitwa kwa kiyahudi Bethabàra
maana yake ni pahala pa kukatisha, pahala pa kusimama na kuangalia kwa mbali au nyumba
ya Bwana. Yaonekana kwamba pahala alisimama Musa juu ya mlima Nebo na kutafakari nchi
ya ahadi na kuona ni pahala gani ambapo angewaingiza wayahudi katika nchi ya ahadi.
Kwa bahati mbaya yeye mwenyewe hakuingia, badala yake Yoshua ndiye aliyeliingiza taifa
katika nchi ya ahadi.
Bethbara iko karibu sana na ziwa la mauti. Yesu anavuka
mto na kuingia nchi Takatifu kuanza kufanya kazi ya kuhubiri na hatimaye kwenda kuteswa
na kufa na kufufuka. Maelezo ya kiteolojia ya pahala hapa, kwamba yabidi kujiruhusu
kuongozwa na Yesu toka nchi ya utumwa wa dhambi na kuingia katika nchi ya uhuru kamili
wa kiroho.
Kabla ya kubatizwa, Yesu alibadilishana kauli kidogo na Yohane aliyekuwa
anakataa. Kwa hoja kwamba kumbatiza huko kungeonesha kuwa Yesu ni mdhambi aliye mbali
na Mungu. Yesu anasema: “Kubali hivi sasa, kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki
yote.” Hapa Yesu anataka kumwambia Yohane kuwa anayo picha tofauti ya haki yaani,
haki anayoijua Yohane ni tofauti na haki ile ya Yesu.
Haki ya Mungu anayotaka
kuiingiza Yesu duniani ni ile inayowakomboa na kuwapenda watu wote. Yohane anakubali
na kumfanya Yesu avuke mto kwenda nchi ya ahadi yaani nchi ya uhuru. Kuingia huko
kwa Yesu katika nchi ya Ahadi (Galilaya) ni kama kule kwa kutoka Misri alikokimbili.
Sasa inaamana ya kuingia tena katika nchi ya Misri ya maisha yetu, yaani nchi ya utumwa
wakaao Farao wanaotukandamiza na kunuonea. Sasa mkombozi anatujia na kutukomboa. Yesu
ni Musa mpya.
Siku ile ya ubatizo wa Yesu pale Yordani kuna vituko vitatu vinavyoweza
kutufundisha. Mosi, tunaambiwa kwamba mara tu baada ya kubatizwa, Yesu anapotoka majini
anga linafunguka. Maelezo yake ni ya kihistoria ya mahusiano ya Mungu na binadamu.
Kwamba, hapo mwanzo karibu katika karne kama tatu hivi, Mungu alikuwa anaongea na
watu kwa njia ya manabii aliokuwa anawatuma kwao. Baadaye, akaacha kutuma manabii
kwa sababu watu hawakuwa tena wanawasikiliza.
Mungu akafunga mbingu zake zilizokuwa
saba. Watu wakabaki wanateseka, wakalalamika kwamba hatuna tena nabii, itakuwaje,
tutatambuaje mawazo ya Mungu kama hakuna nabii? Unaona sasa kwa mara nyingine Yesu
anapoibuka toka majini, anga linafunguka. Milango ya mbingu zote saba inafunguka.“Bwana
ulikuwa na haki ya kutukasirikia, maana tulitenda dhambi; Lakini sasa, Ee Bwana, wewe
u baba yetu; sisi tu udongo, nawe u mfinyanzi wetu, sisi sote ni kazi ya mikono yako.
Ukifungua mbingu tutaokoka”. (Isaya 64). Kwa ujio wa Yesu, hatuhitaji tena nabii kwani
tunaye Mungu hapahapa “Emmanueli”.
Pili, tunasikia kwamba Roho ya Mungu akamshukia
Yesu kama njiwa. Njiwa huyo anatukumbusha Agano la Kale, baada ya tufani kuu, alitumwa
njiwa kuangalia gharika kuu, baadaye anarudi akiwa na tawi la mzeituni mdomoni. Njiwa
ni alama ya wema, uzuri, unyofu. Ndivyo Yesu anavyofika. Baada ya Tufani, Mungu anasema,
sitaharibu tena nchi. Hakutakuwa tena tufani itakayoharibu nchi, bali atatuma roho
aliye alama ya uzima mpya. Ndivyo sasa Yesu anapoibuka toka majini roho anaingia duniani.
Tatu, sauti ikasikika toka mbinguni. Sauti inayomtambua Yesu. Sauti inatambua
kitendo kinachofanyika. Yaani ufunuo au epifania ya Mungu. Sasa ni wakati rasmi Mungu
anapoanza shughuli yake mpya. Kwa hiyo anapoibuka toka majini, Mungu anatamtambua
kuwa ndiye mwanae mpenzi. Mwana anafanana na wazazi wake katika sifa na thamani zote
muhimu, hata namna ya kuongea na kutenda mambo. Sisi tumwangalie mwanae anayefanana
na Mungu, nasi tutakuwa na roho hiyohiyo kwani tunafanana na Baba. Wote ni watoto
wa Mungu, Yeye ni mwanae wa pekee mpendwa kwani ameleta habari njema ya upendo, na
ya haki kwa watu wote.
Tujikubali kwamba tuko katika nchi ya utumwa mwa dhambi,
tugeuke kwa kuvuka Yordani pamoja na Yesu, tutaibuka na roho wa Bwana, aliye roho
wa unyenyekevu, upole, wema, upendo na haki. Roho atakayetupa nguvu ya kushinda majaribu
ya maisha magumu ya humu jangwani (ulimwenguni). Kisha tutaibuka kidedea katika maisha
mapya pamoja na Kristu Mfufuka. Yesu anatuagiza kutenda mambo yote kwa kufuata mfano
wa maisha yake. Ndivyo alivyowaagiza mitume wake siku ya karamu ya mwisho, “fanyeni
hivi kwa kunikumbuka mimi.” Sasa twende tukakiangalie chumba ambacho Yesu alifanya
sherehe mara ya mwisho hapa duniani na kuyatamka maneno hayo.
“FANYENI HIVI
KWA UKUMBUSHO WANGU.” Lk 22:19
Karibu Wainjili wote wanatupatia maelezo
ya karamu ya mwisho. Katika chumba kilicho juu. Wainjili wanasema kwamba karamu hiyo
ilikuwa ya Agano Jipya na la milele. Katika mazingira hayohayo ya kula Yesu akawaosha
miguu wafuasi wake. Kila mwenjili anajitahidi kutoa fundisho la pekee kadiri anavyoona
yeye. Hapa sisi tufuate maelezo ya mwinjili Luka. Sote tunafahamu kilichotokea siku
ile ya karamu ya mwisho. Maneno ambayo Luka anayoyatumia na ambayo yabidi kuyafanyia
tafakuri ni yake tunayoyasikia katika kila misa: “fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.”
Ni mwinjili Luka peke yake anayesema maneno hayo.
Lengo la Yesu lilikuwa ni
kuwaalika wafuasi wake wote kumkumbuka Yeye, yaani daima kurudia kufanya kitendo hicho.
Lakini zaidi pia aliwataka wamege mkate na kula ikiwa kama alama ya msingi katika
imani yetu. Tendo la kumega mkate ni ufupisho wa maisha yake yote toka kuzaliwa hadi
kufa kwake. “Mimi nimejifanya chakula ili kuyalisha maisha.” Ni kama vile angekuwa
Bethlehemu inayotembea (mobile bakery). Luka anataka kutuambia kuwa mnapokuwa katika
karamu hii, au mnapokula chakula hiki, mnafanya uchaguzi kama wangu wa kujitoa na
kujitolea. Huo ni mwaliko wa kuwa kama Kristu, wa kuwa mkate na kujigawa kwa wengine.
Kwa hiyo haitaeleweka kabisa kumwona mkristu baada ya kuadhimisha ekaristi, anashindwa
kusaidia wengine.
Hali halisi nyingine inayoonekana humo chumbani, wakati
wa sherehe hiyo kuliibuka mabishano mazito hasahasa tungeweza kuyaita mahojiano makali
kati ya mitume. Kisa walikuwa wanabishana juu ya ukuu, juu ya kuwa na heshima na cheo
kati yao “ni nani anayehesabiwa kuwa mkuubwa.” Yesu akawaambia: “Wakuu wa mataifa
huwatawala, na wenye mamlaka juu yao huitwa Wenye fadhili; lakini kwenu ninyi sivyo;
bali aliye mkubwa kwenu na awe kama aliye mdogo; na mwenye kuongoza kama yule atumikaye.
Mimi niko kati yenu kama atumikaye.” Haya tena ni maneno yanayoletwa na Luka peke
yake wakati huu wa mlo. Ni maneno kwa ajili ya kila mtu hasahasa yule anayejiita mkristu.
Hayo ndiyo mambo yanayoharibu jumuia za kiristu siku za leo. Kazi ya mtu aliyeshiba
ni kutafuta cheo.
Mahojiano hayo ya mitume hayakuishia kwao tu. Mabishano hayo
yameletwa hapa kuonesha kuwa yanaweza kumpata kila mmoja katika maisha yake. Hasa
kuhusu kujihoji wewe mwenyewe kuhusu kuchagua mambo. Hali kadhalika Yesu Kristu katika
maisha yake hapa duniani alikabiliwa na changamoto hii ya kujihoji nafsini mwake.
Mahojiano hayo ya Yesu tutayaona baada ya karamu ya mwisho akiwa kwenye mlima wa Mizeituni.
Tunaambiwa kuwa alipatwa na uchungu sana ambao katika Injili ya Kiswahili
wanafasiri kuwa ni dhiki. “Yesu akatoka akaenda mpaka mlima wa Mizeituni kama ilivyokuwa
desturi yake; ...akajitenga na mitume wake… huko akasali... kwa vile alikuwa katika
dhiki... hari yake ikawa kama matone ya damu yakidondoka nchi.” Alikuwa katika katika
dhidi au tuseme alikuwa na hali mbaya sana. Yaani ni kama hali ile anayokuwa nayo
mtu kabla ya kufa. Neno hili uchungu pia limetokea katika injili ya Luka peke yake,
kwa kiingereza ni ”Agony”. Maana halisi ya neno hilo agoni lamaanisha mapambano,
mashindano au mahojiano makali. Hasa mashindano kama yale ya wanariadha. Yesu aliingia
katika mashindano kama hayo.
Toka mwanzo wa maisha yake, Yesu ilimbidi aingie
katika mapambano na mashindano na nguvu za shetani. Mapambano hayo hayakwisha katika
vishawishi, yaani pale shetani alipomjia Yesu jangwani mara tu baada ya kubatizwa.
La hasha, baada ya vishawishi vile tunasikia kuwa shetani alimwacha Yesu kwa muda.
“Basi alipomaliza kila jaribu, Ibilisi akamwacha akaenda zake kwa muda.” (Lk. 4:13).
Shetani anakuja tena akijua kwamba hapa sasa ni lala salama! Hapa kuna mapambano
makali ya roho yanayomdai Yesu kuwa mwaminifu na inabidi kuyashinda. Yesu anashinda!
Kuonesha kwamba hayo yalikuwa ni mashindano makali, Yesu anatoka jasho, hilo kama
vile jasho linalomtoka mwanariadha wakati wa mashindano. Kwa hiyo agoni siyo uchungu
bali ni mapambano, kuvutana, ukinzani, ugomvi ndani ya mtu. Mapigano yaliyoko ndani
ya mtu.
Katika mapambano hayo Yesu anajiandaa kwa kujitenga na kusali. “Mwenyewe
akajitenga nao kama kiasi cha kutupa jiwe, akapiga magoti akaomba.” Anajiweka katika
mahusiano na Mungu ili kuweza kuiona mipango ya Mungu. Anajiweka katika mahusiano
na Mungu, ili kujua Mungu anao mpango gani kwa ajili yake. Yesu alisali sana na akawahimiza
mitume wake kukesha na kusali. “Alipofika mahali pake aliwaambia: ‘ombeni kwamba msiingie
majaribuni. Ondokeni, mkaombe msije mkaingia majaribuni.”
Sala inamsaidia
Yesu. Kisha wanafika malaika kumliwaza. Hiyo ni alama ya kuwa na mawazo ya ndani ya
Mungu. Endapo alifikiria kutoroka maisha, kutoroka mateso sasa anaimarika, na kuhiari
kuurekebisha ulimwengu. Kwa hiyo ili kushinda mapambano ya ndani ya mtu, yabidi kusali
sana. Kuunganisha mipango yako na mipango ya Mwenyewe Mungu. Hatima Ndugu zangu
wahiji au ma-alhaji, nimejaribu kuwapatieni picha ndogo sana ya sehemu atakazoenda
kuhiji Papa, ili uweze kutanguzana naye kiroho. Sehemu hizo ni ile aliyozaliwa Yesu
hapa duniani, nikitumia kauli mbiu “Twendeni mpaka Betlehemu”, kisha Yordni sehemu
aliyobatizwa, tungeweza kusema aliyosimikwa rasmi kama nabii mtangazaji wa habari
njema baada ya kushinda majaribu jangwani. Halafu tumeona chumba cha mwisho alichoweka
karamu ya mwisho na kuwaagiza mitume wake “Fanyezi hivi kwa ukumbusho wangu.” Sehemu
hizi tatu, ni kama mzunguko wa maisha ya binadamu hapa duniani, ambayo ni kuzaliwa,
kazi na kufa.
Tofauti ya mzunguko wa maisha yetu na ya Yesu ni kwamba, Yesu
anaanza maisha yake (kama mkate ulioshuka toka mbinguni) akishuhudiwa na Mungu Baba
kwa njia ya malaika, anaanza kazi yake akishuhudiwa na Mungu Baba (kwa sauti) na Roho
Mtakifu (kwa mfano wa njiwa). Anakufa na kufufuka kisha anaendelea kukaa pamoja nasi
Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.” Yaani sasa imebaki kuwa kazi kwetu kuishi maisha
kama alivyoishi Yesu.
Ikiwa kama nyongeza katika ramani hii ya hija, ningependa
kuwadokezea mambo mawili, mosi, nadhani umewahi kuusikia msemo unaosema kwamba, Nchi
Takatifu ni Injili ya Tano. Ningependa kukuhakikishia kwamba msemo huo ni wa kweli
kabisa. Ukienda na kuona nchi ya kibiblia kwa macho yako, utaweza kushabikia vizuri
zaidi Maandiko Matakatifu. Jiografia ya nchi itakuonesha wapi historia ya ukombozi
ilitokea katika Biblia. Mang’amuzi utakayopata yatakupa picha ya hadithi unazozisoma
katika Biblia.
Pili, utasikia watu wanaamkiana wakilitumia amkio lilelile
alilolitumia sana Yesu alipokuwa anawatokea mitume wake baada ya ufufuko. “Amani kwenu”.
Amkio hilo linatumika hadi leo katika maamkio ya kawaida kwa lugha ya kiyahudi shalom.
Anza kufanya mazoezi ya kulitamka neno hilo, na cha muhimu zaidi ni kuliishi neno
hilo Amani katika maisha yako yote. Mwisho, ni kwamba Nchi ya Ahadi ndiyo aliyoishi
Yesu aliyeitwa na Yohane Mbatizaji “Huyu ndiye Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi
za dunia”. Huyo Mwanakondoo anamgeukia kila mmoja wetu na kumwalika kukaa naye kama
alivyowaalika wale wanafunzi wawili waliokuwa wanamfuata akawauliza: “Mnatafuta nini?”
Wakamwambia, “Rabi (maana yake Mwalimu), unakaa wapi?” Akawaambia, “Njoni, nanyi mtaona.”
Wakaenda, wakaona akaapo, wakakaa kwake siku ile.” (Yoh. 1:37-39) Tunaalikwa sote
kufanya hija ndani ya mioyo yetu ambayo ni makao ya Roho Mtakatifu na tukae na Yesu
daima. Imeandaliwa na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.