Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Ulaya, CCEE, linawaalika waamini
pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuungana na Baba Mtakatifu Francisko kwa sala
wakati wa hija yake ya kitume Nchi Takatifu kwa ajili ya kuwaimarisha ndugu zake katika
imani, matumaini na mapendo, kwa kuonesha ukaribu na mshikamano wa kidugu na wananchi
wote huko Mashariki ya Kati.
Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani
Ulaya linawapongeza Wakristo ambao licha ya hali ngumu wanayokabiliana nayo, lakini
bado wameendelea kuwa ni mashahidi wa imani ya Kikristo. Hija ya Baba Mtakatifu Francisko
ni hija ya kiekumene na Makanisa yote ya Kikristo, ili kwa pamoja yajielekeze zaidi
katika mchakato wa ujenzi wa umoja na mshikamano wa Kanisa pamoja na kuendelea kulinda
na kutunza maeneo matakatifu; mahali alipoteswa, kufa na kufufuka Kristo!
Ujumbe
wa amani utakaotolewa na viongozi wa Makanisa uwe ni kikolezo kwa viongozi wa kisiasa
huko Mashariki ya Kati kuongeza juhudi za kutafuta na kudumisha misingi ya haki, amani
na utulivu, ili hatimaye, amani ya kudumu iweze kupatikana!