2014-05-22 09:49:50

Papa Francisko anataka kuwasha tena moto wa majadiliano ya kiekumene!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na Kituo cha Televisheni cha Vatican anabainisha kwamba, hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko katika Nchi Takatifu itakayomwezesha kutembelea Amman, Bethlehemu na Yerusalemu kuanzia tarehe 24 hadi tarehe 26 Mei 2014, itakuwa ni kuasha tena moto wa majadiliano ya kiekumene. Kilele cha hija hii ya kitume ni pale Baba Mtakatifu Francisko atakapokutana na kusali pamoja na Patriaki Bartolomeo wa kwanza kwenye Kaburi Takatifu.

Hija hii ya kitume anasema Kardinali Parolin ni sehemu ya maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 tangu Mtumishi wa Mungu Papa Paulo VI alipokutana, akazungumza na kusali na Patriaki Anathegoras wa Costantinopoli, huu ukawa ni mwanzo mpya wa majadiliano ya kiekumene ndani ya Kanisa.

Hija ya Baba Mtakatifu inajikita katika misingi ya majadiliano ya kiekumene na kidini; umuhimu wa kujikita katika mchakato wa haki na amani sanjari na kuangalia nafasi na dhamana ya Wakristo katika Nchi Takatifu, kwani hawa wanapaswa kushiriki kikamilifu katika kuchagia ustawi na maendeleo ya maeneo yao kama kielelezo makini cha uwepo endelevu wa Kristo kati ya watu wake!

Kardinali Pietro Parolin anasema kwamba, hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko ni chemchemi ya furaha na faraja kwa Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema wanaoishi huko Mashariki ya Kati. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumsindikiza kwa njia ya sala katika hija hii ya kiekumene ambayo pia inajikita katika mshikamano wa kidugu kati ya watu!







All the contents on this site are copyrighted ©.