2014-05-22 11:53:30

Miaka 50 ya kuzaliwa! Zawadi Kituo cha Televisheni!


Bwana Robert Olagunju kutoka Nigeria kama sehemu ya maadhimisho ya Miaka 50 tangu kuzaliwa kwake ameamua kuanzisha kituo cha Luninga kitakachojulikana kama "Lumen Christi", yaani "Mwanga wa Kristo" kitakachorusha matangazo yake ndani na nje ya Nigeria bila malipo.

Matangazo haya yataanza kutolewa kwa lugha ya Kiingereza na maandishi kwenye lugha ya Kifaransa. Mikakati iko mbioni kuhakikisha kwamba, matangazo haya pia yanapatikana kwa njia ya maandishi kwa lugha ya Kihispania, Kireno, Kiswahili na Kipidgin.

Lengo la kuanzisha kituo hiki chenye mwelekeo wa Uinjilishaji Mpya Barani Afrika ni kumshukuru Mungu kwa kumwezesha kufikisha miaka 50 tangu alipozaliwa na kama alama ya shukrani, basi anataka kuanzisha kituo cha Televisheni ili kusaidia mchakato wa Uinjilishaji Barani Afrika. Bwana Olagunju anatambua sadaka kubwa iliyoko mbele yake na anasema anataka kuivalia njuga, ili kutekeleza ndoto yake.

Kituo hiki kitarusha matangazo yake kwa kipindi cha masaa 24 kwa siku. Anaomba ushirikiano na mshikamano kutoka kwa waamini na viongozi wa Kanisa ili kutimiza ndoto yake kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa Barani Afrika.







All the contents on this site are copyrighted ©.