2014-05-22 10:07:12

Boko Haram inataka kuisambaratisha Nigeria


Askofu mkuu Ignatius Ayau Kaigama, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria anasema mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa na Kikundi cha Boko Haram nchini Nigeria yanaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao pamoja na kugumisha majadiliano ya kidini yaliyokuwa yamekwishafikiwa nchini humo katika mchakato wa kudumisha misingi ya haki, amani na mshikamano wa kitaifa!

Majadiliano ya kidini na kiekueme yalikuwa yameanza kushika kasi ya ajabu kwa watu kushirikiana na kushirikishana mipango na mikakati ya maendeleo. Anasema, hivi karibuni alifanya hafla kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa Kanisa kuu la Huruma ya Mungu, tukio ambalo liliwashirikisha waamini wa dini mbali mbali ambao wamechangia kwa hali na mali! Haya ndiyo majadiliano ya kidini yanayojengeka katika maisha ya watu na wala si mashambulizi, kinzani na migongano ya imani inayotokana na baadhi ya watu kuwa na misimamo mikali ya kidini.

Boko Haram inalenga kuitekeleza Nigeria kutokana na mashambulizi yake ya mara kwa mara, changamoto kwa Serikali kuwasaka na hatimaye kuwatia pingu wahusika wa mashambulizi haya yanayotekelezwa kwa ajili ya mafao binafasi. Serikali inawajibu wa kuwaambia wananchi wa Nigeria sababu za mashambulizi haya kama yanafumbata masuala ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kidini, ili mwarobaini wa kweli uweze kuchemshwa na watu kupatia ili kukata mzizi wa vita na mashambulizi ya kigaidi nchini Nigeria. Serikali ina dhamana ya kulinda maisha na mali ya wananchi wake nchini Nigeria.







All the contents on this site are copyrighted ©.