Wanawake jitokezeni kimasomaso kujenga Kanisa na Jamii!
Wajumbe wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, hivi karibuni wameshiriki katika mkutano
mkuu wa Baraza la Wanawake wa Kimethodist, kwa kuwataka Wanawake Wakristo kushiriki
kikamilifu katika ujenzi wa Makanisa na Jamii. Changamoto hii imetolewa na Hillary
Clinton, aliyekuwa Katibu mkuu wa Nchi wa Marekani wakati alipokuwa anachangia hoja
katika mkutano mkuu wa wanawake wa Kimethodisti.
Anasema,
wanawake wanapaswa kujifunga kibwebwe ili kupambana na changamoto mbali mbali zinazoendelea
kujitokeza katika ulimwengu wa utandawazi, ambako wanawake na wasichana wanaendelea
kunyanyasika; kuna ukosefu mkubwa wa usawa kati ya watu, utu na heshima ya binadamu
vinadhalilishwa kutokana na biashara haramu ya binadamu pamoja na ukosefu huduma makini
ya afya kwa mama na mtoto.
Mkutano huu uliwajumuisha wanawake 7, 000 walioshiriki
kwenye kituo cha kimataifa cha mikutano huko Kentucky, Marekani. Baraza la Wanawake
wa Kimethodisti limekuwa mstari wa mbele katika kuwajengea wanawake uwezo wa kushiriki
katika maendeleo ya Kanisa na Jamii inayowazunguka tangu ilipoundwa kunako mwaka 1953.
Katika kipindi cha miaka sitini, Baraza la Makanisa Ulimwenguni linasema bado
kuna umuhimu wa kuwajengea wanawake uwezo ili waweze kuwa na vyama vyenye nguvu vitakavyosaidia
kuharakisha ujenzi wa misingi ya haki, amani na usawa kati ya watu. Wanawake waimarishwe
kiroho ili waweze kuwa na utashi wa kufanya maamuzi makubwa katika maisha yao. Mkutano
mkuu wa wanawake wa Kimethodisti ulikuwa ni fursa ya kusali, kuabudu na kushirikishana
mang’amuzi mbali mbali ya maisha ya kijamii.
Wajumbe wameangalia athari za
utumwa mamboleo kutokana na ushuhuda uliotolewa na wahanga wa biashara haramu ya binadamu
na nyanyaso za watoto wadogo, wanaofanyishwa kazi za suluba kwa ujira kidogo, lakini
madhara yake ni makubwa katika makuzi na maendeleo ya watoto hawa kwa sasa na kwa
siku za usoni. Bado kuna makundi makubwa ya wanawake na watoto yanayoendelea kutumbukizwa
katika biashara ya ngono ya kimataifa. Hawa ni watu wanaopaswa kusaidiwa ili kutambua
utu na heshima yao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Upendo
kwa Mungu na jirani ndiyo urithi mkubwa ambao wanawake wanaweza kusaidia kuchangia
katika malezi na majiundo ya watoto wao. Wanawake waoneshe ujasiri kwa kuwashinikiza
wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kutekeleza sera na mikakati ya Kimataifa inayopania
kudbiti uchafuzi wa mazingira, kwani madhara yake ni makubwa mno katika uso wa dunia.
Ni
jukumu la wanawake Wakristo kusimama kidete kulinda na kutetea zawadi ya uhai tangu
pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti yanapomfika kadiri ya
mpango wa Mungu, dhidi ya utamaduni wa kifo. Wanawake wajengewe uwezo wa kupambana
na changamoto zinazoendelea kuibuka katika medani mbali mbali za maisha, kwa kuwapatia
elimu makini na uwezo wa kiuchumi pamoja na kuwashirikisha katika vikao vinavyotoa
maamuzi.
Wanawake wamepongezwa kwa kuendelea kutunza familia ambazo zimeathirika
kutokana na athari za ugonjwa wa Ukimwi. Wajumbe, kimsingi wanasema kuna haja kwa
Jumuiya ya Kimataifa kujenga uchumi unaojikita katika haki, mshikamano na udugu.