Misimamo mikali ya kidini ni kati ya changamoto kubwa zinazotishia amani, utulivu
na usalama katika nchi nyingi Barani Afrika. Vita na kinzani za kijami zinazoendelea
kujitokeza sehemu mbali mbali Barani Afrika zina chanzo chake katika misimamo mikali
ya kidini, hali ambayo imepekea hata kuwepo pia kwa mashambulizi ya kidaidi.
Kumbe,
kuna haja kwa Serikali na viongozi wa dini Barani Afrika kushirikiana kwa pamoja ili
kuondokana na tatizo la watu wenye misimamo mikali ya kiimani ambao wanaendelea kuwa
ni tishio katika kudumisha misingi ya haki, amani na utulivu. Ni changamoto iliyotolewa
na Rais Ismail Omar Guelleh wa Gjibout alipokuwa anazungumza na wakuu wa dini ya Kiislam
kutoka Gjibout, Ethiopia, Sudan, Somalia, Yemen na Saud Arabia waliokuwa wanajadili
tatizo la misimamo mikali ya kidini Afrika Mashariki.
Baadhi ya viongozi wa
dini ya Kiislam wanasema, leo hii kutokana na vitendo vya mashambulizi ya kigaidi
kutokana na misimamo mikali ya kiimani sanjari na vitendo vya kigaidi, kuna tafsiri
mbali mbali zinazotolewa pengine hata kinyume cha ukweli wa dini ya Kiislam, hali
ambayo inachafua dini ya Kiislam katika ujumla wake kutokana na vitendo vya watu wachache
ndani ya Jamii.