2014-05-21 08:34:41

Tumetoka mbali katika majadiliano ya kiekumene!


Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la kuhamasisha umoja wa Wakristo anasema, hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Nchi Takatifu ni mwendelezo wa mchakato wa majadiliano ya kiekumene ulioanzishwa na Papa Paulo VI pamoja na Patriaki Anathegoras wa Yerusalemu miaka hamsini iliyopita.

Viongozi hawa wawili walionesha ujasiri na ushupavu wa imani kwa kutaka kulinasua Kanisa kutoka katika usiku wa giza la kinzani na migawanyiko, tayari kuanza mchakato wa umoja miongoni mwa Wakristo baada ya "patashika nguo kuchanika" katika kipindi cha miaka 525!

Viongozi hawa wakakutana mjini Yerusalem, mji wenye maana kubwa kihistoria na kiimani, hapa ni chemchemi ya imani ya Kikristo, ili kuanza kumwilisha wosia wa Yesu, ili wote wawe wamoja chini ya mchungaji mkuu ambaye ni Yesu Kristo mwenyewe!

Huu ukawa ni mwanzo wa hija ya majadiliano ya kiekumene yanayosimikwa katika ukweli, upendo na utofauti, ili kwa pamoja waweze kuwa ni mashahidi wa Injili ya Kristo. Papa Paulo VI na Patriaki Anathegoras wanatambulika na Mama Kanisa kuwa ni viongozi wa majadiliano na manabii wa upendo wa kiekumene. Tangu wakati huo, mchakato wa majadiliano kati ya Makanisa na ndani ya Makanisa yenyewe ambayo bado yamegawanyika ukaanza kwa kasi ya ajabu.

Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ukaendeleza dhamana hii kwa mwelekeo na mwono mpya zaidi, dhamana ambayo imetekelezwa na Mapapa wote tangu baada ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kwa kujikita katika majadiliano ya upendo na ushuhuda wa pamoja unaomwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa. Umoja wa Kanisa utafikia kilele chake pale Wakristo watakapofanikiwa kuadhimisha kwa pamoja Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa anasema Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI.

Majadiliano ya kiekumene yameendelea kuwa ni chachu ya kusafisha dhamiri, ili kuanza hija ya pamoja inayosimikwa katika msamaha na upatanisho wa kweli baada ya Makanisa kutengana kunako mwaka 1054. Utengano ndani ya Kanisa katika kipindi cha miaka 50 iliyopita na alama ya upendo ikaanza kushika kasi na kumwilishwa katika mahusiano ya kidugu, majadiliano ya kitaalimungu na uelewa mpana kati ya Makanisa haya mawili, kazi kubwa iliyofanywa na Mtakatifu Yohane Pauli II katika maisha na utume wake tangu kunako mwaka 1979.

Kardinali Kurt Koch anasema kati ya Mwaka 1980 hadi mwaka 1990 juhudi kubwa za kiekumene zilielekezwa katika kuimarisha misingi ya imani ya Kikristo, kwa kuangalia mambo msingi yanayoyaunganisha Makanisa haya mawili: Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Sakramenti ya Daraja Takatifu zikapewa tafakari ya kina.

Mwaka 1990 hadi mwaka 2000 majadiliano ya kiekumene yalishika kasi zaidi lakini yakaingiliwa na ugumu kwa baadhi ya Makanisa kufukua madonda ya utengano yaliyokuwa yamejionesha ndani ya Kanisa kwa kudhani kwamba, umoja wa Kanisa ulipania kuyameza baadhi ya Makanisa na hivyo kutoweka katika ramani ya kimataifa. Hapa majadiliano ya kiekumene yakagonga mwamba kwa masikitiko makubwa!

Kardinali Kurt Koch anakiri kwamba, ni juhudi za Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI zilizokwamua hali hii mgando ya majadiliano ya kiekumene na hivyo kuanza tena lakini mwiba mkubwa wa majadiliano haya ni "Nafasi na Ukuu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro ndani ya Kanisa na umuhimu wa Sinodi". Hapa Makanisa yakatambua kwamba, kuna haja ya kuendeleza majadiliano ya upendo katika ukweli.

Dhana hii inafanyiwa kazi kwa sasa na Papa Francisko na kwa namna ya pekee kwa mara ya kwanza katika historia ya Kanisa, Patriaki Bartolomeo wa kwanza alipomtembelea Papa Francisko mjini Vatican. Hija ya Baba Mtakatifu Francisko Nchi Takatifu ni kutaka kuimarisha huduma ya kiekumene ndani ya Kanisa, kwa kutambua kwamba, umoja wa Kanisa ni zawadi kutoka kwa Roho Mtakatifu.

Imehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.