Paji la elimu liwasaidie kumwona Mungu katika yote!
Baba Mtakatifu Francisko katika Katekesi zake anazotoa kila Jumatano ametafakari kuhusu
Mapaji Saba ya Roho Mtakatifu, yaani: Hekima, Akili, Ushauri na Nguvu, Elimu, Ibada
na Uchaji wa Mungu. Jumatano tarehe 21 Mei 2014, Baba Mtakatifu Francisko ametafakari
kuhusu paji la elimu zawadi inayomwezesha mwamini kwa njia ya kazi ya uumbaji, kupokea
ukuu na upendo wa Mungu na mahusiano yake ya dhati na kila binadamu na kutenda kadiri
ya mapenzi yake.
Baba Mtakatifu anasema, kwa njia hii, watu wanaweza kuona:
uzuri, ulinganifu na wema wa viumbe vyote vinavyomzunguka mwanadamu kwa kutumia jicho
la Mwenyezi Mungu ambaye ndiye Muumbaji wa vyote. Kama inavyojionesha katika maisha
ya Mtakatifu Francisko wa Assis na kwa watakatifu wengi, Paji la Elimu linamwezesha
mwamini kufikia kiwango cha hali ya juu kabisa cha tafakari kuhusu asili ya dunia
na hatimaye kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa furaha.
Mwelekeo unaotolewa
na paji hili la maisha ya kiroho anasema Baba Mtakatifu, linawawezesha watu kuheshimu
zawadi ya uumbaji na kutawala rasilimali ya dunia kwa hekima na uwajibaki zaidi kwa
ajili ya mafao ya familia yote ya binadamu. Huu ni mwaliko wa kuwa na mwono mpana
zaidi si tu katika watu na vitu vya dunia hii na kusahau kwamba katika utaratibu wake,
thamani na uzuri wake unamwelekea Mwenyezi Mungu, kama kiini na hitimisho lake.
Baba
Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumwomba Roho
Mtakatifu ili awasaidie kukuza ndani mwao Paji la Elimu, ili liweze kuwasaidia kuona
upendo wa Mungu unaoiongoza dunia na kujibu kwa moyo wa shukrani na sifa kwa Mwenyezi
Mungu mwingi wa wema na upendo usiokuwa na mipaka.
Baba Mtakatifu ametambua
uwepo wa mahujaji kutoka Jimbo Katoliki la Pointe Noire, Congo Brazaville na Afrika
ya Kusini. Anawataka waamini kushuhudia upendo wa Mungu kwa kuumwilisha katika matendo
ya huruma kwa jirani zao. Waamini wawe na ujasiri wa kuona chapa ya uwepo wa Mungu
kwa kila kiumbe chake, ili kutambua utupu wa mtu na hatimaye kuungama ukuu wa Mungu.
Mwezi Mei uwawezeshe waamini kuimarisha imani yao pamoja na kuendelea kumtumainia
Bikira Maria. Anawaomba kumwombea ili aweze kuifanikisha hija yake ya kichungaji huko
Nchi Takatifu. Anawaomba waamini kudumisha Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, kwa
kutoa kipaumbele cha kwanza kwa uwepo wa Mungu katika hija ya maisha yao ya kila siku.