2014-05-20 09:39:40

Vatican inazidi kuimarisha sheria na mikakati ya kupambana na uhalifu katika fedha!


Taarifa ya Mamlaka ya Habari za Fedha mjini Vatican, AIF katika taarifa yake kwa Mwaka 2013 inaonesha kwamba, vyombo vya sheria vimeimarishwa kushiriki katika mapambano dhidi ya makosa ya jinai katika masuala ya fedha. Kumekuwepo na ushirikiano mkubwa katika uwanja wa kimataifa kiasi kwamba udhidbiti wa Mamlaka ya Fedha umeboreka zaidi.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Vatican, Siku ya Jumatatu tarehe 19 Mei 2014, Bwana Renè Brulhart, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Habari za Fedha mjini Vatican anasema, tathmini iliyofanywa na Kamati ya wataalam wa masuala ya fedha kutoka Ulaya, Moneyval, Mwezi Desemba 2013 kuhusu mikakati iliyochukuliwa ili kudhibiti utakatishaji wa fedha na ufadhili wa vitendo vya kigaidi, inaonesha kwamba, Mamlaka ina muundo madhubuti katika kuzuia na kupambana na makosa ya jinai katika masuala ya fedha.

Taarifa ya mzunguko wa fedha iliyotiliwa mashaka imeongezeka maradufu tangu mwaka 2012 hadi mwaka 2013, hii ni kutokana na weledi, umakini na ufuatiliaji wa masuala ya fedha kwa kushirikiana na mamlaka mbali mbali. Mamlaka ya Habari za Fedha inaendelea kushirikiana na nchi pamoja na mamlaka mbali mbali ili kudhibiti uhalifu katika masuala ya fedha. Watu wanaanza kujenga utamaduni wa ukweli na uwazi kwa kuzingatia sheria zilizopo.

Mabadiliko yaliyofanywa na Baba Mtakatifu Francisko katika masuala ya fedha kwa nyaraka tatu muhimu yamesaidia kujenga nguzo kuu mbili kwa ajili ya kusimamia na kupata habari za masuala ya fedha, ili kuimarisha mikakati ya utawala bora na utekelezaji wa majukumu kwa kuzingatia kanuni, maadili na weledi. Ukaguzi uliofanywa kwenye Benki ya Vatican, IOR, unaonesha kwamba, kanuni na sheria zilizowekwa zinaweza kuzuia na kudhibiti utakatishaji wa fedha na ufadhili kwa vitendo vya kigaidi.







All the contents on this site are copyrighted ©.