2014-05-20 09:41:14

Papa Francisko: Jengeni umoja na mshikamano; saidieni familia na maskini!


Kwa mara ya kwanza katika historia ya Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 19 Mei 2014 amefungua mkutano wa sitini na sita kwa kuwataka kutambua kwamba, wao ni wachungaji wa Jumuiya ya Kristo Mfufuka. Wao ni wachungaji wa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa, wachungaji wanaoendeleza ujio wa Ufalme wa Mungu kati ya watu kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa familia, maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake ya ufunguzi amewataka Maaskofu Katoliki Italia kushikamana na Kristo pamoja na Kanisa lake, ili aweze kuwaimarisha katika imani, matumaini na mapendo, kwa kuendelea pia kuwa ni waaminifu katika utekelezaji wa mapenzi ya Mungu katika maisha na utume wao.

Kanisa ni Jumuiya ya Kristo Mfufuka inayojikita katika imani ambayo inarutubishwa kwa Neno na Sakramenti za Kanisa, changamoto na mwaliko wa kuepukana na vishawishi vinavyoweza kuwasonga na hivyo kushindwa kutekeleza wajibu wao kikamilifu: kwa kutokuwa na mikakati makini ya kichungaji, kwa kujiamini sana na kutoona umuhimu wa kumtegemea Kristo katika maisha na utume ndani ya Kanisa. Baba Mtakatifu anawaalika Maaskofu kumtegemea Kristo na kumkaribisha ili aweze kutenda pamoja nao, ili waweze kuwa kweli ni watakatifu na mifano bora ya kuigwa.

Maaskofu ni wachungaji wa Kanisa ambalo ni Fumbo la Mwili wa Kristo, linalowashirikisha kwa namna ya pekee Fumbo la Pasaka na huduma inayowawajibisha kujenga na kudumisha umoja, upendo, mshikamano na ukarimu, bila kumezwa na malimwengu wala kuwadharau wengine. Huu ndio mfano bora uliooneshwa na Watakatifu Yohane XXIII na Yohane Paulo II.

Mama Kanisa anapojiandaa kumtangaza Mtumishi wa Mungu Papa Paulo VI hapo tarehe 29 Oktoba 2014 kuwa Mwenyeheri, Maaskofu wanakumbushwa maneno yake aliyowataka Maaskofu Katoliki Italia kujisadaka kwa ajili ya ujenzi wa umoja wa kitaifa, kwa kuondokana na udhaifu unaoweza kujitokeza kwa kutokuwa na mawasiliano makini, kwani kinzani na utengano ndani ya Kanisa ni kashfa kubwa na hakuna mtu anayeweza kuhalalisha kitendo hiki.

Baba Mtakatifu anawakumbusha kwamba, umoja na mshikamano wao unapata chimbuko lake katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu; kwa kujenga na kudumisha amani na utulivu hata katika nyakati ngumu. Tasahufi ya Ekaristi takatifu inajenga mshikamano, majadiliano, udugu, uhuru na uwezo wa mtu kuchangia kadiri ya Roho Mtakatifu anavyowakirimia. Baraza la Maaskofu linapaswa kuwa ni kwa ajili ya huduma ya umoja, mahusiano ya dhati, mahali pa kubadilishana na kushirikishana mang'amuzi na changamoto katika shughuli za kichungaji.

Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu kuwa karibu na Mapadre wao katika maisha na utume wao; kwa kuwapatia majiundo makini ya awali na endelevu katika maisha ya kiutu, kitamaduni, kiroho na kimahusiano. Mkutano mkuu wa Baraza la Maaskofu utakaofanyika mwezi Novemba, 2014 utajikita katika maisha ya Mapadre, changamoto ya kufanya maandalizi makini.

Maaskofu wawasaidie watawa kutekeleza utume wao ndani ya Kanisa na kuishi kadiri ya kweli za Kiinjili, ili waweze kuwa ni mashahidi wa Injili ya Furaha. Maaskofu wajenge utamaduni wa kusikiliza watu wao, wawaimarishe katika imani, wawasaidie waamini walei katika maisha na utume wao wa kuyatakatifuza malimwengu. Wawapatie mikakati itakayowawezesha waamini walei kutangaza Neno la Mungu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao na Katekesi. Utume wa Kanisa unajikita katika umoja na upatanisho kama kielelezo cha unabii katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, matendo ya huruma ni muhimu sana katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu kati ya watu. Kanisa liguswe na matatizo yanayowakabili watu katika hija ya maisha yao hapa duniani, lisaidie kupambana na ukosefu wa haki msingi za binadamu. Kanisa linatumwa kutangaza ukweli kuhusu Kristo na huruma kwa waja wake, kwa kutambua kwamba, upendo katika ukweli ni kikolezo cha maendeleo endelevu katika familia ya binadamu, tunu zinazopaswa kumwilishwa katika matendo!

Maaskofu wawe ni wachungaji wasiomezwa na malimwengu, watu wanaopenda na kuishi ufukara, kwa kuonesha huruma na unyenyekevu katika maisha. Wawe ni watu huru wanaweza kuwakaribia watu kwa upendo na kuwasindikiza wale wanaotembea katika upweke na giza la uvuli wa maisha, ili hatimaye watu hawa waweze kuonja tena utu, matumaini pamoja na kuwa na maisha mapya.

Hapa Familia zinapaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha tunu bora za maisha ya kifamilia. Familia ni kiini cha Jamii na ushuhuda wa uzuri wa maisha. Hapa ni mahali ambapo watu wanapaswa kufundishwa namna ya kukumbatia Injili ya Uhai, kwa kuwasaidia wazazi katika mchakato wa malezi ya watoto wao, kwa kuwaganga wale waliopoteza dira na mwelekeo wa maisha.

Baba Mtakatifu Francisko anawaambia Maaskofu wa Italia kwamba, waoneshe mshikamano wa upendo na watu wasiokuwa na fursa za ajira au wale ambao wamepoteza ajira kutokana na sababu mbali mbali, watu ambao kwa sasa maisha na utu wao uko mashakani. Wawafungulie milango wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta faraja na kutaka kusalimisha maisha yao kutoka kwenye vita, nyanyaso na dhuluma, kwani upendo ni kielelezo kikuu cha ushuhuda wa ukarimu, kwa njia hii Injili itaenea sehemu mbali mbali kwa kuonesha mvuto na mashiko!

Baba Mtakatifu anasema kuna haja ya kuwa na sera mbadala katika mikakati ya maendeleo ya kiuchumi kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na mahitaji yake msingi, kwa kulinda na kuboresha mazingira sanjari na kuwajengea watu matumaini wakati huu wanapopambana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa; mmong'onyoko wa kimaadili na utu wema pamoja na watu kupoteza mwelekeo katika maisha ya kiroho. Hapa kuna haja ya kuwa na mikakati makini kwa kuona ukweli wa mambo, ili kujenga na kudumisha, udugu na mshikamano.

Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewaomba Maaskofu wa Italia kumsindikiza katika hija yake ya kitume huko Nchi Takatifu, kama sehemu ya maadhimisho ya jubilee ya Miaka 50 tangu Papa Paulo VI alipokutana, akazungumza pamoja na kusali na Patriaki Anathegoras wa Yerusalemu. Anakwenda huko ili kuwaonjesha mshikamano wa Kanisa kwa ajili ya watu wanaoishi katika eneo ambalo limebarikiwa na Yesu kwa kufa na kufufuka kwake!







All the contents on this site are copyrighted ©.