2014-05-20 09:49:21

Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini lina dhamana ya kujenga urafiki na amani!


Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini, Jumatatu tarehe 19 Mei 2014 limeadhimisha Jubilee ya Miaka 50 tangu lilipoanzishwa na hivyo kuendelea kuwa ni chombo cha ujenzi wa urafiki, amani na maendeleo ya watu sehemu mbali mbali duniani.

Hii ni sehemu ya ujumbe kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko aliomwandikia Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini wakati huu Baraza hili linapoadhimisha Jubilee ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake na Papa Paulo VI hapo tarehe 19 Mei 1964 kama sehemu ya cheche za utekelezaji wa mageuzi makubwa yaliyoletwa na Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kwa kujikita katika majadiliano ya kina na walimwengu.

Baba Mtakatifu anasema, Kanisa halina budi kujielekeza katika majadiliano ya kidini mahali linapopatikana na kuishi. Kanisa lazima lijitahidi kuwa Neno na ujumbe kwa ajili ya mchakato wa majadiliano ili kuwashirikisha watu Injili ya Furaha ya kukutana na Yesu kwa kutambua na kuthamini utambulisho wa Kanisa.

Huu ndio ushuhuda uliooneshwa kwa namna ya pekee na Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili katika maisha na utume wake kwamba: Majadiliano ya kidini na Uinjilishaji ni chanda na pete, kwani yanategemeana na yanapaswa kuendelezwa bila kujichanganya. Hii ni kazi ya Roho Mtakatifu anayelijenga na kulidumisha Kanisa; ni Roho Mtakatifu ambaye pia ni mdau mkuu wa Uinjilishaji anayewakarimia watu mapaji yake pamoja na kuendeleza mchakato wa majadiliano na watu wote.

Baba Mtakatifu Francisko anakumbusha kwamba, Kanisa Katoliki linatambua na kuthamini umuhimu wake katika kuhamasisha urafiki na hali ya kuheshimiana kati ya waamini wa dini mbali mbali na kwamba, Yesu kama alivyofanya kwa Wanafunzi wa Emmau, anaendelea kulisindikiza Kanisa katika njia ya maisha ya kila mwanadamu. Ili watu kuweza kutembea kwa pamoja, kuna haja pia ya kufahamiana na kushirikiana na watu na tamaduni mbali mbali.

Baba Mtakatifu anasema, Kanisa litaendeleza majadiliano ya kidini, kwa njia ya ushirikiano, matunda ambayo tayari yameanza kuonekana pamoja na kuwa na utashi na nia ya kujenga urafiki kwa kushiriki mikutano mbali mbali ya majadiliano.

Mwishoni, Baba Mtakatifu anaungana na Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini katika kuadhimisha Miaka 50 tangu lilipoanzishwa na anatumaini kwamba, litaendelea kutekeleza dhamana na utume wake ili kujenga amani na kusaidia mchakato wa maendeleo endelevu.







All the contents on this site are copyrighted ©.