2014-05-19 10:08:45

Pamoja na Bikira Maria ili kujenga msingi bora wa familia!


Maadhimisho ya Sakramenti ya Upatanisho ilikuwa ni fursa ya pekee kwa waamini kutoka Jimbo kuu la Maputo, Msumbiji walioshiriki katika hija ya maisha ya kiroho kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima, yaliyoko huko Namaacha, kwenye Parokia ya Mama Yetu wa Fatima kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao. Hija hii imeongozwa na kauli mbiu "Pamoja na Bikira Maria tujenge thamani ya familia", ambayo kilele chake kilikuwa ni hapo tarehe 18 Mei 2014 kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa na Askofu mkuu Francisko Chimoio wa Jimbo kuu la Maputo!

Kuanzia tarehe 15 Mei, 2014 waamini kutoka sehemu mbali mbali za Jimbo kuu la Maputo na Majimbo mengine jirani walianza kumiminika kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima ili kusali Rozari Takatifu, Kuabudu Ekaristi Takatifu, Njia ya Msalaba pamoja na Ibada ya kuungama kama sehemu ya mchakato wa kujiandaa kupokea neema na baraka zinazotolewa na Mama Kanisa katika maadhimisho kama haya!

Lengo la hija hii ya maisha ya kiroho, lilikuwa ni kuwaimarisha waamini katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; kwa kukazia umuhimu wa malezi makini na kina katika familia ili kuwajengea watoto msingi thabiti wa imani kwa Kristo na Kanisa lake. Malezi bora ni chachu na chemchemi ya miito mitakatifu ndani ya Kanisa anasema Askofu mkuu Chimoio katika mahubiri yake.

Askofu mkuu Chimoio amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai na kuwataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda na kutetea zawadi ya uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Huu ni mwaliko kwa waamini kupinga utamaduni wa kifo kwa nguvu zao zote.

Amewakumbusha waamini kwamba, hija ni tendo la toba na imani, linalopania kumkirimia mwamini neema na baraka katika maisha yake, ili aweze kukua na kukomaa katika fadhila ya imani, matumaini na mapendo kwa Mungu na jirani, sanjari na kusimama kidete kulinda, kutetea na kujenga misingi bora ya maisha ya ndoa na familia.

Askofu Chimoio amewataka waamini kuwa na jicho la huruma na mapendo kwa jirani na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, kwa kujitahidi kumwilisha imani katika matendo, ili iweze kuzaa matunda kwa kuanzia ndani ya familia. Waamini wanapaswa kutambua kwamba, Familia zao ni Kanisa dogo la nyumbani, mahali ambapo Mwenyezi Mungu anatukuzwa na mwanadamu anatakatifuzwa kwa njia ya matendo adili na manyofu. Familia zinapaswa kujenga na kudumisha fadhila ya msamaha na upendo kama chachu ya amani na matumaini kati ya watu!

Waswahili wanasema "eti furaha haina madaraka", wimbo wa shukrani, uliwainua waamini wote kutoka katika Parokia 43 za Jimbo kuu la Maputo zilizoshiriki katika hija kwenye Madhabahu ya Bikira Maria, Mama Yetu wa Fatima ambayo kwa Mwaka 2014 yanaadhimisha Miaka 70 tangu yalipojengwa. Tukio hili limeiachia Familia ya Mungu Jimbo kuu la Maputo, Msumbiji, chapa ya furaha na matumaini, tayari kujisadaka kwa ajili ya kujenga na kuimarisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa dogo la nyumbani, yaani Familia.

Taarifa hii imeandaliwa na

Sr. Magreth Ngoi, A.S.C.
Msumbiji.







All the contents on this site are copyrighted ©.