Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumamosi tarehe 17 Mei 2014 amemweka
wakfu Askofu mkuu Hubertus Matheus Maria Van Megen, Balozi mpya wa Vatican nchini
Sudan ya Kusini katika Ibada ya Misa Takatifu iliyofanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu
Christopher, Jimboni Roermond, Ireland. Katika mahubiri yake, Kardinali Parolin amemtaka
Askofu mkuu Megen kuwa ni mjumbe wa upatanisho na msamaha wa kweli miongoni mwa wananchi
wa Sudan anapotekeleza dhamana yake kama Balozi wa Vatican nchini humo.
Anasema,
Sudan ya Kusini inakabiliana na changamoto za vita na kinzani za kijamii. Kwa njia
ya maneno, ushuhuda amini na kwa kushirikiana na Maaskofu mahalia, Askofu Megen anatumwa
kuwatangazia wananchi wa Sudan ya Kusini Injili ya Upatanisho, Msamaha na Huruma ya
Mungu pamoja na kuendelea kuiimarisha Jumuiya ya Waamini Sudan ya Kusini, ili iweze
kuwaaminifu kwa Kristo na Kanisa lake, kwa kumwilisha ndani mwao ile Amri kuu ya Upendo
kwa Mungu na jirani.
Askofu mkuu Megen amekumbushwa kwamba, atakuwa ni mhudumu
wa upendo wa Yesu kwa watu wake ili kuonesha utukufu wa Mungu uliojionesha kwa namna
ya pekee, kwa njia ya Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu,
ili kuwaimarisha waamini katika ushindi wa Msalaba dhidi ya dhambi na mauti. Awe ni
uhakika wa sala na maombezi ya Baba Mtakatifu Francisko katika utekelezaji wa dhamana
na majukumu yake huko Sudan ya Kusini. Awe ni mfano mwema wa kiongozi anayeandamana
na Kondoo wake, akisimsikiliza kwa makini Roho Mtakatifu.
Ili kuwa kweli mchungaji
mwaminifu kuna haja anasema Kardinali Parolin kukuza na karama ya toba na wongofu
wa ndani, ukweli na muwazi, anayesimamia umoja na mshikamano wa Watu wa Mungu, tayari
kujisadaka kwa ajili ya mafao ya wengi. Kama Balozi wa Vatican anao wajibu wa kuwaunganisha
watu kiroho na kiakili, ili wote waweze kujisikia kuwa chini ya Khalifa wa Mtakatifu
Petro, kwa kuwaimarisha ndugu zake katika imani, uaminifu katika Injili na utume wa
Kanisa.
Kama mwakilishi wa Baba Mtakatifu nchini Sudan ya Kusini, atawajibika
kupandikiza mbegu ya haki na amani kama chachu ya kukuza na kuendeleza Ufalme wa Mungu
kati ya watu wa mataifa, kwa kutambua kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya watu waliojipatanisha
na kujipyaisha ndani ya Kristo. Askofu mkuu Megen amewekwa chini ya ulinzi na usimamizi
wa Mtakatifu Josephina Bakhita, binti kutoka Sudan na shahidi wa neema na huruma ya
Mungu inayoleta mageuzi makubwa katika maisha ya mwanadamu.
Ibada hii ya Misa
Takatifu imehudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Kanisa pamoja na Serikali ya Ireland.