Miaka 50 imegota tangu Mtumishi wa Mungu Papa Paulo VI alipoanzisha Baraza la Kipapa
la Majadiliano ya Kidini, kama sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kidini kati ya
Wakristo na waamini wa dini mbali mbali duniani, ili kulinda, kujenga na kudumisha
misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati kati ya watu wa mataifa.
Ilikuwa ni
Siku kuu ya Pentekoste, tarehe 17 Mei 1964, Papa Paulo VI alipoanzisha Sekretarieti
ya majadiliano ya kidini, leo hii ni Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini linaloongozwa
na Kardinali Jean Louis Tauran.
Baraza hili lilikuwa na dhamana ya kuendeleza
majadiliano ya kidini , ili kuwapatia watu wengi zaidi nafasi ya kusikiliza Habari
Njema ya Wokovu kwa njia ya majadiliano ya kidini; dhamana iliyoboreshwa zaidi na
Mtakatifu Yohane Paulo II katika maisha na utume wake. Kipindi cha miaka hamsini iliyopita,
kimekuwa ni fursa muafaka kabisa ya majadiliano ya kidini yanayosimikwa katika ukweli,
ushirikiano wa dhati pamoja na kutafuta njia muafaka za kuweza kujenga na kuimarisha
amani na utulivu duniani.
Kardinali Jean Louis Tauran anasema, Baraza lake
limebahatika kukutana na watu mbali mbali waliojitosa kwa ajili ya kukoleza majadiliano
ya kidini kati ya watu. Baraza limekuwa pia ni msaada mkubwa katika kukoleza majadiliano
ya kidini kwenye Makanisa mahalia. Huu ni mchango mkubwa uliotolewa na viongozi mbali
mbali waliobahatika kuongoza Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini tangu kuundwa
kwake.
Papa Yohane XXIII wakati alipokuwa anafungua rasmi maadhimisho ya Mtaguso
mkuu wa Pili wa Vatican alikazia umoja kati ya watu wa mataifa unaojikita katika dhana
ya kuheshimiana na kuthaminiana; kwa kusimamia misingi ya ukweli na kanuni maadili;
utu na heshima ya binadamu na kwamba, Kanisa liwe ni mdau mkubwa wa majadiliano ya
kidini kati ya watu, kwa kuwa ni “Neno na Ujumbe”. Waamini watambue na kuheshimu tunu
msingi za maisha ya kiroho, kimaadili na kiutu zinazopatikana kwenye dini nyingine
duniani. Kwa pamoja waamini wa dini mbali mbali wasimame kidete kutetea uhuru wa kuabudu;
wajitahidi kujenga utamaduni wa mshikamano na udugu kati ya watu, ili waweze kusaidiana
kwa dhati.
Papa Yohane Paulo wa kwanza katika utumishi wake wa siku thelathini
na mitatu tu, kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, alilitaka Kanisa kushirikiana na watu
wote wenye mapenzi mema, wanaosimamia haki, wa kweli na wanyofu wa moyo ili kuondokana
na vita pamoja na matumizi ya nguvu yanayopelekea mateso makubwa kwa watu wasiokuwa
na hatia.
Kardinali Tauran anasema, Papa Yohane Paulo II ndiye aliyeotesha
mizizi ya utamaduni wa majadiliano ya kidini, akathubutu kunako tarehe 27 Oktoba 1986
kuwakutanisha viongozi wakuu wa kidini mjini Assisi, ili kusali kwa ajili ya kuombea
amani duniani sanjari na maadhimisho ya Mwaka wa Amani Duniani.
Matukio ya
kigaidi ya tarehe 11 Septemba 2001 yalichafua hali ya hewa kiasi kwamba, mahusiano
ya kidini yakapwaya kwa kunyoosheana kidole. Papa Yohane Paulo II akatoa kanuni za
kudumisha misingi ya amani duniani. Alibahatika katika hija zake za kitume kutembelea
na kukutana na waamini wa dini ya Kiislam katika Misikiti yao, kama alivyofanya tarehe
6 Mei 2001 mjini Damasko.
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI aliendeleza
majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali ili kujenga na kuendeleza urafiki
kati ya watu wa mataifa, daima wakitafuta mafao ya wengi. Kanisa linatambua kwamba,
lina dhamana ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu, kwa kujadiliana na kushirikiana
na watu wote wenye mapenzi mema. Ulimwengu wa utandawazi ni fursa makini ya kujenga
na kudumisha udugu na mshikamano kati ya watu.
Kardinali Tauran anasema, Baba
Mtakatifu Francisko katika uongozi wake wa kipindi cha mwaka mmoja, amekwisha kutana
na kuzungumza na makundi ya waamini wa dini mbali mbali, lengo ni kuendeleza urafiki
na hali ya kuheshimiana. Tarehe 7 Septemba 2013 aliwaalika waamini wa dini mbali mbali
kufunga na kusali pamoja naye kwa ajili ya kuombea amani huko Mashariki na kwa namna
ya pekee nchini Syria. Waamini wa dini mbali mbali walishiriki katika utekelezaji
wa wito huu.
Hivi ndivyo Mtumishi wa Mungu Paulo VI alivyojitahidi kujadiliana
na Ulimwengu, Yohane Paulo II akajenga utamaduni wa majadiliano kwa njia ya amani
na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI akajikita katika majadiliano ya upendo katika
ukweli na katika maadhimisho ya miaka hamsini ya mchakato wa majadiliano ya kidini,
Papa Francisko anawachangamotisha waamini kujenga majadiliano ya urafiki kwa kukutana
na watu.
Kardinali Jean Louis Tauran anasema, majadiliano ya kidini ni changamoto
endelevu ndani ya Kanisa, inayopaswa kujikita katika ujasiri, hekima, uvumilivu na
udumifu, daima kwa kuendelea kumtumainia Roho Mtakatifu, kama alivyofanya Papa Paulo
VI wakati wa maadhimisho ya Pentekoste kwa Mwaka 1964, hapo ukawa ni mwanzo wa Baraza
la Kipapa la majadiliano ya kidini. Mchakato wa majadiliano bado una njia ndefu na
umesheheni changamoto nyingi!
Habari hii imeandaliwa na Padre Richard A.
Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.