2014-05-19 07:52:00

Matatizo ndani ya Kanisa yanatatuliwa kwa njia ya upembuzi yakinifu, majadiliano na sala!


Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake wakati wa Sala ya Malkia wa mbingu, Jumapili tarehe 18 Mei 2014 anasema, Liturujia ya Neno la Mungu, inaonesha matatizo yaliyojitokeza kwenye Jumuiya ya Wakristo wa mwanzo, baada ya Kanisa kukua na kuongezeka kadiri ya mapenzi ya Kristo na hivyo, kufungua mipaka kwa watu kutoka tamaduni nyingine.

Hali hii ilisababisha manung'uniko kama inavyojitokeza hata leo katika baadhi ya Parokia. Maskini, wajane na yatima wa Kiyunani walisahauliwa katika huduma msingi zilizokuwa zinatolewa, Waebrania wakapewa upendeleo wa pekee. Katika hali kama hii anasema Baba Mtakatifu, Mitume waliamua kulivalia njuga tatizo hili kwa kukutana na kujadili kwa pamoja, kwa kutambua kwamba, kulikuwa na tatizo lililokuwa linahitaji kupatiwa ufumbuzi. Hapa viongozi wa Kanisa na waamini wanajadiliana na hatimaye, kugawana majukumu katika Kanisa.

Mitume wakaamua kujikita katika kutangaza Neno la Mungu na Sala na Mashemasi saba waliochaguliwa wakapewa dhamana ya kuhudumia mezani pamoja na kuwasaidia maskini. Hawa ni watu waliochaguliwa kwa sababu ni watu waliokuwa waaminifu, wenye imani na wamejaa Roho Mtakatifu pamoja na kuwa na hekima. Mashemasi hawa wakaombewa na Mitume. Hali ikawa shwari na Kanisa likasonga mbele.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, matatizo na changamoto mbali mbali ndani ya Kanisa zinatatuliwa kwa njia upembuzi yakinifu, majadiliano na sala, kwa kutambua kwamba, umbea, wivu na kijicho ni mambo ambayo hayana tija wala mashiko kwa ustawi na maendeleo ya Kanisa na kamwe hayataweza kuleta amani na utulivu. Waamini hawana budi kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kuwaongoza katika mchakato wa kufikia umoja, amani na utulivu kwa kuheshimu na kuthamini zawadi na karama mbali mbali zilizoko ndani ya Kanisa.

Mara baada ya Sala ya Malkia wa mbingu, Baba Mtakatifu Francisko aliyaelekeza mawazo yake huko Serbia na Bosnia ambako zaidi ya watu thelathini walifariki maji baada ya kukumbwa na mafuriko na wengine zaidi ya elfu kumi na tano hawana makazi baada ya nyumba zao kusombwa na mafuriko, mwishoni mwa juma. Baba Mtakatifu amewahakikishi uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala.

Baba Mtakatifu amemkumbuka pia Mwenyeheri Askofu Anton Durcovic, shahidi wa imani, mchungaji mwaminifu na jasiri, aliyeuwawa kikatili na utawala wa kinazi kunako mwaka 1951. Baba Mtakatifu anaungana na waamini wa Jimbo la Ias na Romania katika ujumla wake kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa kulijalia Kanisa mwamini shujaa na shupavu katika imani.







All the contents on this site are copyrighted ©.