Jumuiya ya Kimataifa inashutumu adhabu ya kifo kwa Meriam kutoka Sudan
Hukumu ya adhabu ya kifo iliyotolewa kwa Meriam Yahya Ibrahim Ishaq kutoka Sudan kwa
kuolewa na Mkristo raia wa Sudan ya Kusini, inaendelea kupingwa katika majukwaa ya
kimataifa, kiasi kwamba, habari hizi zimemfikia Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana
Ban Ki-Moon. Wakili wa Mama huyu amekata rufaa na kwa sasa wanasubiri uamuzi kutoka
kwa Mahakama kuu ya Rufaa kutoa majibu.
Mama huyu ambaye amezaa mtoto mmoja
na ana mimba kwa sasa anasema tangu awali amekuwa ni Mkristo na wala hajawahi hata
siku moja kuwa mwamini wa dini ya Kiislam. Wakati huo huo, Serikali ya Sudan inasema
kwamba, ina dhamana ya kusimamia haki msingi za binadamu na uhuru wa kidini kadiri
ya Katiba ya nchi ya Mwaka 2005 pamoja na sheria za nchi.
Ufafanuzi huu umetolewa
na Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Sudan baada ya kupata shinikizo kutoka katika
Jumuiya ya Kimataifa kuhusu uvunjwaji wa haki msingi za binadamu na uhuru wa kuabudu!