2014-05-19 12:26:54

Jifungeni kibwebwe kutangaza Habari Njema ya Wokovu!


Baba Mtakatifu Francisko amewataka waamini kumtegemea Roho Mtakatifu katika mchakato wa Uinjilishaji mpya, kazi iliyoanzishwa na Kristo mwenyewe, changamoto iliyosimamiwa na kuendelezwa na Mtakatifu Paulo. Mitume wakajaliwa kutenda miujiza kudhihirisha uwepo endelevu wa Kristo kati ya watu wake. Hili ni tukio ambalo liliwashangaza wapagani wakadhani kwamba, Mwenyezi Mungu amewatembelea kwa ujio wa Paulo na Barnabas, wakataka kuwatolea sadaka!

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, Jumatatu, tarehe 19 Mei 2014 anasema, mitume hawakukatishwa tamaa na madhulumu waliyokumbana nayo katika hija ya maisha yao, wakapiga moyo konde na kuendelea kumtangaza Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu. Ni watu waliotenda kwa kusukumwa na imani, wakashuhudia jinsi watu walivyolipokea Neno la Mungu na kutendewa miujiza.

Baba Mtakatifu anasema, katika Injili Yesu anawaambia wafuasi wake kwamba, wakimpokea Roho Mtakatifu atawafundisha na kuwakumbusha yote aliyowafundisha, mwaliko kwa waamini kumkimbilia Roho Mtakatifu waliojaliwa wakati walipopokea Sakramenti ya Ubatizo na kuimarishwa katika Kipaimara. Roho Mtakatifu anawakirimia waamini nguvu na neema ya kusonga mbele ili kutangaza ujumbe wa wokovu kama alivyofanya Mtakatifu Paulo.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuchunguza dhamiri zao ili kuangalia mahali ambapo moyo wao umejikita, ili waweze kuwa na ujasiri wa kumtolea Kristo ushuhuda wa imani katika matendo, bila kujificha wala kuwa na woga. Uchunguzi wa dhamiri ni hatua muhimu sana katika hija ya maisha ya kiroho, kwa kutambua kwamba, wamepewa zawadi ya Roho Mtakatifu anayewaongoza katika maisha yao ya kiroho.







All the contents on this site are copyrighted ©.