Changamoto katika ujenzi wa misingi ya haki, amani na upatanisho!
Patriaki Beshara Rai wa Kanisa la Wamaronite kutoka Lebanon anatarajiwa kushiriki
katika hija ya kichungaji itakayofanywa na Baba Mtakatifu Francisko katika Nchi Takatifu
kuanzia tarehe 24 hadi tarehe 26, Mei 2014 na inayoongozwa na kauli mbiu, ili wote
wawe wamoja!
Taarifa zinaonesha
kwamba, hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa dini kutoka Lebanon kutembelea
Yerusalemu, tangu mwaka 1948. Hii ni changamoto ya ujenzi wa misingi ya haki, amani
na upatanisho kati ya mataifa, kwa kukazia mafao ya wengi, uhuru na mshikamano wa
kimataifa katika kukabiliana na changamoto za maisha ya watu.
Itakumbukwa
kwamba, Lebanon na Israeli ni nchi ambazo bado zinaangaliana kwa “macho ya makengeza”
kiasi kwamba, wananchi wa Lebanon hawaruhusiwi kutembelea eneo la Israeli. Kadiri
ya sheria za Israeli, viongozi wa Kanisa wanaruhusiwa kutembelea Israeli ili kutoa
huduma kwa waamini wapatao 10, 000 wa Kanisa la Maronite.
Patriaki Beshara
Rai anasema, hija ya kiekumene itakayomwezesha kukutana na Baba Mtakatifu Francisko
pamoja na viongozi wengine wa Makanisa ni hija ya kidini na wala haina uhusiano wowote
na masuala ya kisiasa.