Mtumishi wa Mungu Askofu Anton Durcovic aliyezaliwa kunako tarehe 17 Mei 1888 nchini
Austria ametangazwa Mwenyeheri na Kardinali Angelo Amato kwa niaba ya Baba Mtakatifu
Francisko, huko Bucarest, tarehe 17 Mei 2014.
Akizungumzia kuhusu tukio hili,
Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa
wenyeheri na watakatifu anasema kwamba, Baba yake mzazi alifariki dunia akiwa na umri
wa miaka sita na hivyo kulazimika kwenda kuishi na Mama na Kaka yake nchini Romania.
Akasoma mjini Bucarest na Roma na kufanikiwa kupata cheti za uzamivu katika masomo
ya falsafa na taalimungu.
Mwenyeheri Durcovic alipadrishwa kunako Mwaka 1910
na kwa miaka mingi akajisadaka kufundisha dini shuleni na shughuli za kichungaji Parokiani.
Kunako Mwaka 1947 akateuliwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Ias lililoko Romania na
kuwekwa wakfu kunako Mwezi Aprili 1948. Hapa akaanza kujitosa bila ya kujibakiza kwa
ajili ya shughuli za kitume kwa kutembelea Parokia pamoja na kuwaimarisha ndugu zake
katika Kristo ili waweze kuwa jasiri na imara katika imani.
Mwenyeheri Anton
Durcovic anaongeza idadi ya Maaskofu na Mapadre kutoka Romania waliokwishatangazwa
na Mama Kanisa kutokana na uaminifu wao kwa Kristo na Kanisa lake, kiasi hata cha
kuyamimina maisha yao,ushuhuda wa hali ya juu wa imani katika matendo. Romani ni nchi
ambayo imebahatika kuwa na Mashahidi wengi wa imani. Itakumbukwa kwamba, Mwezi Agosti
2013, Padre Vladimir Ghika alitangazwa kuwa Mwenyeheri. Hawa ni Mashahidi wanaoendelea
kulipamba Kanisa.
Baba Mtakatifu Francisko katika barua yake ya kitume anamtaja
kuwa ni mchungaji jasiri, mtume wa Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu na shahidi jasiri
wa umoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Mwenyeheri Anton Durcovic alikuwa ni mpenda
amani, mtu mwenye imani, mapendo na huruma. Alionesha upendo wa pekee kwa maskini
na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa Jamii. Jimboni mwake, kulikuwa na maskini
wengi wa hali na kipato. Kwa kuguswa na mateso na mahangaiko ya watu wake, akaamua
kufungua ukumbi wa chakula kwenye Shule ya Notre Dame de Sion kwa ajili ya maskini
waliokuwa wanaishi mjini hapo.
Mashahidi wanasema kwamba, Mwenyeheri Anton
Durcovic alibahatika kupendwa na wengi na wala hakuwa na maadui wala kutafutwa na
wanasiasa, kwani kwake wote waliokuwa ni ndugu zake na kwamba, maneno yake yalikuwa
ni chachu ya Injili na kwamba, alisema na kutenda yote kama Kristo mwingine na daima
aliona madhulumu na mateso yakiandama maisha yake.
Kardinali Angelo Amato anasema,
tarehe 26 Juni 1949 Askofu Anton Durcovic alikamatwa na kikosi cha usalama kwa kuhatarisha
Ukomonisti, licha ya kuonesha unyenyekevu na hekima katika maisha yake. Hii ni siku
ambayo alikuwa amepanga kutoa Sakramenti ya kipaimara kwa vijana 650 katika Parokia
moja iliyokuwa pembeni mwa Jiji la Bucarest.
Akiwa njiani kwa miguu kuelekea
Parokiani hapo, alikamatwa na vyombo vya usalama na kupotea bila kujulikana mahali
alipokuwa, akawa anahamishwa kutoka gereza moja hadi jingine. Huko akateswa na kudhulumiwa
sana, alikuwa ananyimwa maji na chakula, unyama wa binadamu! Huu ni ushuhuda uliotolewa
na baadhi ya wafungwa wenzake waliobahatika kutoroka magerezani. Alitengwa na wafungwa
wenzake, akafungiwa kwenye chumba cha kifo na hivyo kufariki dunia kati ya tarehe
10 na 11 Desemba 1951. Mwili wake ukachukuliwa na dereva na kwenda kuzikwa kwenye
makaburi ya pamoja.
Kardinali Angelo Amato anasema, fundisho kubwa linalotolewa
na Mwenyeheri Anton Durcovic ni kuwa na nguvu na wajasiri katika majaribu, kwa kutambua
kwamba, upendo wa Kristo bado unawasindikiza hata katika madhulumu na mateso kama
haya na kwamba, baada ya Ijumaa kuu kuna Pasaka, yaani ufufuko wa Bwana.
Mwenyeheri
Anton Durcovic amekuwa kweli ni mfano wa kuigwa ndani na nje ya Romani. Bado anaendelea
kukumbukwa na Familia ya Mungu Jimbo kuu la Bucarest na Jimboni kwake Ias. Hawa ni
watu walioimarishwa katika maisha yao ya kiroho kiasi kwamba, wakaanza hija ya kutafuta
utimilifu wa maisha ya Kiinjili. Ni kiongozi aliyeonesha utakatifu wa maisha kati
ya watu wake!